Main Title

source : Parstoday
Jumanne

10 Januari 2023

15:39:41
1337456

Matukio muhimu sana na ya kuamua hatima kuhusiana na vita vya Yemen

Matukio mawili mapya yamejiri kuhusiana na vita vya Yemen, ambayo kila moja ni muhimu na lina taathira kubwa ya kuamua hatima ya vita hivyo.

La kwanza ni jitihada za Harakati ya Ansarullah za kutaka kuhitimisha hali ya Si Vita Si Suluhu, ambayo imekuwa ikitawala nchini Yemen kwa takriban miezi mitatu sasa tangu ulipokoma kurefushwa muda wa usitishaji mapigano. Wakati hali hiyo inaonekana kukidhi maslahi ya madola vamizi ya Saudi Arabia na Muungano wa Falme za Kiarabu-Imarati, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Magharibi, huku kila moja kati ya pande hizo zikiitumia hali iliyopo kwa manufaa yake, Serikali ya Uokovu wa Kitaifa na wananchi wa Yemen hawanufaiki kwa namna yoyote ile na mazingira hayo ya sasa ya Si Vita Si Suluhu; na kwa sababu hiyo, hivi karibuni na sambamba na kutangazwa na serikali ya uokovu wa kitaifa inayoongozwa na harakati ya Ansarullah sera ya kuhitimisha hali hiyo, wananchi wa Yemen wamefanya maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi kuunga mkono sera hiyo huku kaulimbiu yao muhimu zaidi katika maandamano yao ikiwa ni "Mzingiro ni Sawa na Vita".

Takwimu za vifo na maafa ya roho za watu yaliyosababishwa na vita vya miaka minane ilivyotwishwa Yemen, na vilevile za uharibifu uliosababishwa na vita hivyo zinaonyesha kuwa, maafa ya roho za watu yaliyotokana na mzingiro ni makubwa zaidi kuliko maafa ya moja kwa moja yaliyosababishwa na mapigano ya kijeshi; na wakati idadi ya watu waliouawa moja kwa moja kutokana na vita imetajwa kuwa ni 47,000, watu zaidi ya laki tatu wamefariki dunia kutokana na madhara ya mzingiro, wengi wao wakiwa ni watoto wadogo.

Kwa mujibu wa ripoti kamili ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa miezi michache iliyopita, imekadiriwa kuwa jumla ya Wayemeni laki tatu na 77,000 wamepoteza maisha kutokana na uvamizi wa kijeshi dhidi ya nchi yao, ambapo asilimia 70 miongoni mwao ni watoto wa umri chini ya miaka mitano. Aidha, kulingana na ripoti ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, karibu asilimia 60 ya vifo, ikiwa ni sawa na watu 226,000 wamefariki kwa sababu zisizo za moja kwa moja kama maradhi yanayoweza kutibika au kukosa chakula, maji na huduma za afya. UNDP inakadiria kuwa endapo vita vya Yemen vitaendelea hadi mwaka 2030, kiwango cha maafa ya roho za watu kitaongezeka kwa Wayemeni milioni moja na laki tatu kupoteza maisha kutokana na vita hivyo.

Tukio la pili muhimu linalohusiana na vita vya Yemen ni kutangaza Saudi Arabia, tena kupitia mrithi mwenyewe wa ufalme wa nchi hiyo Mohammad bin Salman, kwamba iko tayari kuondoka Yemen mkabala na kupatiwa hakikisho la usalama na harakati ya Ansarullah. Tukio hili limejiri baada ya serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen inayoongozwa na harakati hiyo ya muqawama kutoa muhula mfupi na wa haraka, wa kutaka lijulikane moja, kuhusu uhitimishaji wa hali iliyopo ya Si Vita Si Suluhu. Kwa mujibu wa gazeti la Al-Akhbar muhula huo uliotolewa na serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen unahusu ama kufikiwa suluhu ambayo itakidhi masharti ya serikali hiyo au kuanzishwa vita vitakavyohakikisha masharti yake hayo yanatekelezwa.

Masharti hayo manne ni Mosi: Kuondolewa mzingiro. Pili: Kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Yemen. Tatu: Kufidiwa hasara. Na nne: Kuondoka katika ardhi ya Yemen. 

Kwa mujibu wa ripoti ya Al-Akhbar, mpira sasa uko upande wa Saudia, kwa sababu Sana'a inaitakidi kuwa mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammad bin Salman anao uwezo wa kuyapatia majibu mengi ya masharti hayo.

Hii leo Saudi Arabia, baada ya mafanikio iliyopata nchi ndogo jirani yake ya Qatar kwa kuandaa mashindano ya soka ya kombe la dunia na kutajwa kama mfano wa kuigwa wa "mafanikio" na kutokana na ushindani inaopata kwa Imarati, jirani yake mwingine na mshirika wake katika vita vya Yemen, katika upeo wa kiuchumi na kibiashara duniani, imefikia hitimisho kwamba vita hasa inavyokabiliana navyo ni "Vita vya Rasilimali na Uchumi".

Inavyoonekana, Saudia na hasa bin Salman mwenyewe, hivi sasa amefikia hitimisho kwamba kuendelea vita vya Yemen ni kwa madhara ya nchi yake, ikiwa ni sawa na methali isemayo: 'kuepuka madhara ni sawa kupata tijara'. Lakini suali linaloulizwa ni je, Marekani, na zaidi utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, ambao tokea awali ulichangia kumchochea Bin Salman na Bin Zayed waanzishe uvamizi dhidi ya Yemen, zitairuhusu Saudia na Bin Salman atafakari upya uamuzi wake na kuyaepuka madhara hayo na kupata tijara au la?.../

342/