Main Title

source : Parstoday
Jumatano

11 Januari 2023

16:58:30
1337781

Meja Jenerali Salami: Adui analenga kuvuruga utulivu wa Waislamu kwa kuvunjia heshima matukufu yao

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), akizungumzia hatua ya kudhalilisha ya chapisho la Kifaransa la Charlie Hebdo, alisema kuwa adui sasa analenga kuvunjia heshima matukifu ya Kiislamu ili kuvuruga utulivu wa Waislamu.

Kwa mujibu wa IRNA, Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema hayo jana Jumanne, katika hafla ya kumuenzi na kumtambulisha kamanda wa Kituo cha  Kieneo cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kilichofanyika huko Zahedan. Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wakuu wa koo, viongozi wa kidini, wanazuoni wa Shia na Sunni, familia za mashahidi, na maafisa wa mkoa, Jenerali Salami alisema kwamba adui aliharibu miji ya Iraq, Syria, Afghanistan na Yemen na kuongeza kuwa adui anakusudia kuifanya Iran ikabiliwe na hali hiyo hiyo kwa kuleta mgawanyiko.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alifafanua kuwa, iwapo adui anahisi kwamba anaweza kuanzisha migogoro ya umwagaji damu nchini Iran kwa kueneza mbegu za migawanyiko, basi anafanya hesabu zisizo sahihi kabisa.
Aidha amesisitiza kuwa, kutokana na ufahamu na busara ya wananchi wa Iran, njama za maadui zitashindwa kwani wameshindwa hadi sasa.

Jarida la dhihaka la Charlie Hebdo hivi karibuni liliandaa shindano la kimataifa la uchoraji kwa lengo la kuchapisha vikatuni vya kutusi na kuwavunjia heshima viongozi wa kidini na kisiasa wa Iran, jambo ambalo liliamsha hasira na ukosoaji mkali dhidi ya jarida hilo pamoja na siasa za chuki za serikali ya Ufaransa dhidi ya Uislamu kwa kisingizio eti cha kutetea uhuru wa kujieleza. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilimwita balozi wa Ufaransa mjini Tehran, Nicolas Roche, na kumtaka awafikishie viongozi wa Paris malalamiko ya Tehran kuhusu kitendo hicho cha matusi.

342/