Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

16 Januari 2023

18:12:40
1339032

Makumi ya wanawake watekwa na wanamgambo wenye silaha Burkina Faso

Kwa akali wanawake 50 wametekwa nyara na kundi la wanamgambo wenye silaha nchini Burkina Faso magharibi mwa Afrika.

Duru za usalama zinasema kuwa, wanawake hao wametekwa nyara katika eneo la kaskazini mwa Burkina Faso ambalo limekuwa likishuhudia harakati za makundi ya waasi ambao wamehatarisha usalama na amani katika maeneo hayo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, takriban wanawake 40 walitekwa nyara karibu na eneo la kusini mashariki mwa Arbinda, Alkhamisi, na wengine 20 walitekwa nyara siku Ijumaa kaskazini mwa mji huo. Hiyo ni kwa mujibu wa chanzo ambacho hakikutaka kutajwa. Baadhi yao walifanikiwa kutoroka na kurejea katika vijiji vyao na kutoa taarifa.

Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili wamekimbia makazi yao tangu magaidi hao wakufurishaji waanze kuishambulia Burkina Faso kutokea nchi jirani ya Mali mnamo 2015. 

Zaidi ya theluthi moja ya eneo la nchi hiyo liko nje ya udhibiti wa serikali.

Hujuma na mashambulio ndani ya ardhi ya Burkina Faso yamechochea kuzuka mapinduzi mawili mwaka jana yaliyofanywa na maafisa wa jeshi waliokasirishwa na kuongezeka idadi ya raia wanaouawa katika mashambulio hayo.

Utawala wa kijeshi wa sasa wa Burkina Faso unaongozwa na Kapteni Ibrahim Traore, ambaye akiwa na miaka 34 ndiye kiongozi mwenye umri mdogo zaidi duniani.

342/