Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

16 Januari 2023

18:17:30
1339041

Umoja wa Mataifa walaani mlipuko wa bomu DRC, wataka waliohusika wawajibishwe

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali shambulio lililotokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa moja huko Kasindi, jimboni Kivu Kaskazini na kusisitiza haja ya kuwawajibisha wahusika wa shambulio hilo.

Sambamba na kutoa pole kwa familia zilizofiwa, watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na serikali yao amewatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa katika shambulio hilo la mlipuko kanisani.

Aidha Guterres amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa kupitia Mwakilishi wake Maalumu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, “utaendelea kuiunga mkono Serikali ya DRC na wananchi katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu mashariki mwa nchi hiyo.”

Takriban watu 17 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika shambulio linaloshukiwa kuwa la kigaidi wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa moja la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na shambulio hilo la kigaidi.

Idadi ya wahanga wa shambulio hilo inazidi kuongezeka huku taarifa za karibuni zikisema kuwa, watu 17 wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa. Idadi hiyo ni kwa mujibu wa msemaji wa operesheni ya kijeshi ya Uganda nchini DRC, Bilal Katamba.

Julius Kasake, mmoja wa walioshuhudia tukio hilo amesema, alipokuwa anapita karibu na kanisa hilo ndipo aliposikia mripuko wa kutisha. Amesema watu kutoka nyumba za karibu walikimbilia kanisani hapo ili kuwasaidia wahanga wa mripuko huo.

342/