Main Title

source : Parstoday
Jumatano

25 Januari 2023

19:21:02
1341114

Kanada imezilipa fidia jamii za kiasili kwa sababu haikuwa na budi ila kufanya hivyo

Serikali ya Kanada imeafiki kulipa fidia ya dola bilioni 2.1 kwa waathiriwa wa jamii za kiasili ambao walikabiliwa na mateso katika shule za bweni kwa takriban karne moja.

Fidia hiyo iliamuliwa kufuatia malalamiko ya makundi 325 ya wenyeji wa Kanada na fedha hizo zitawekwa katika mfuko maalumu.

Fidia hiyo itatumika kwa ajili ya jamii za asili za Kanada katika masuala ya elimu, utamaduni na lugha za asili sambamba na kuwasaidia walionusurika, kuwaponya na kuwaunganisha na turathi na utamaduni wao wa jadi.

Garry Feschuk mmoja wa walalamikaji na mmoja wa viongozi wa jamii za asili wa Kanada, anasema: "Ilichukua muda mrefu sana kwa Kanada kuungama kuhusu historia yake chafu na kukubali kwamba mauaji ya kimbari yalijiri na kutambua maafa ambayo jamii zetu ziliyastahamili katika shule za bweni. Sasa umewadia wakati kwa Kanada kufidia hasara na hatua ya sasa ni ya kwanza tu katika mwelekeo huu."

Kuanzia mwishoni mwa karne ya 19 hadi miaka ya 1990, serikali ya Kanada ilipeleka watoto wapatao 150,000 katika shule 139 za bweni. Shule hizo maalumu ziliendeshwa zaidi na Kanisa Katoliki, ambapo watoto waliwekwa mbali na tamaduni, lugha na familia zao. Madhumuni ya kuanzisha shule hizo, ambazo ziliendeshwa na taasisi kadhaa zilizohusishwa na Kanisa Katoliki kati ya 1831 na 1996, yalikuwa ni kuwalazimisha watoto wa jamii za asili kuiga utamaduni wa Kimagharibu au utamaduni wa Wazungu na kuachana na mila zao.

Makumi ya maelfu ya watoto hao wa jamii za asili walihamishwa kwa nguvu kutoka makwao hadi shule hizo na wengi wao walikabiliwa na unyanyasaji, ubakaji na utapiamlo. Ushahidi umebaini kuwa maelfu ya watoto hao walikufa kutokana na magonjwa, utapiamlo na kupuuzwa kwa hali zao. Tume ya Ukweli na Maridhiano katika ripoti ya mwaka 2015, ilisema yaliyojiri katika shule hizo za Kanisa nchini Kanda ni mauaji ya kimbari.

Mamia ya makaburi yasiyo na alama yamegunduliwa katika shule hizo katika muda wa miaka mitatu iliyopita. Suala hili limesababisha kuangaziwa upya na kwa karibu historia chafu ya Kanisa Katoliki katika shule za bweni ilizokuwa inasimamia.

Hivi sasa serikali ya Kanada iko chini ya mashinikizo kwa ajili ya kuchunguza tena na kufidia historia yake ya kikatili ya ukoloni.

Utata wa muda mrefu kuhusu majanga yaliyotokea katika shule hizo uliibuka tena mwaka 2021 baada ya ugunduzi wa mabaki ya watoto 215 katika eneo la shule ya bweni ya shule ya watoto wa jamii za asili katika jimbo la British Columbia magharibi mwa Kanada. Shule hiyo ilikuwa tayari ilishafungwa mwaka  1978. Bado kuna mamia ya maeneo ya makaburi ya umati ambayo hayajagunduliwa ambapo watoto hao walizikwa bila familia zao kujulishwa.

Kanisa Katoliki la Kanada likishirikiana na serikali ya Kanada, liliwapeleka kwa nguvu watoto wa jamii za asili katika shule ambapo watoto walitenganishwa na familia zao na kupelekwa katika shule hizo ambazo kimsingi zilikuwa ni kama kambi  za mateso ili kuwabadilisha kifikra.

Wakazi asili wa Kanada walikuwa wakaaji wakuu wa ardhi hiyo kabla ya wazungu kutoka Ulaya kufika bara Amerika katika karne ya 15, na bado wanaishi ndani ya mipaka ya kisasa ya Kanada. Wakanada hao asili wanajumuisha makundi ya jamii  kadhaa za asili zinazojulikana kama Mataifa Ya Kwanza pamoja na makabila ya Inuit na Métis. Kulingana na takwimu, Kanada ina zaidi ya watu wa jamii za asili wapatao 1,200,000 wanaoishi katika hali mbaya ambapo kiwango cha umaskini, kujiua na uraibu miongoni mwa watu hao ni kikubwa sana.

Kwa hakika, wakazi asili wa Kanada wanakabiliwa na matatizo mengi yanayosababishwa na sera za kibaguzi za serikali ya Kanada. Ubaguzi wa serikali ya Kanada dhidi ya wenyeji wa ardhi hiyo unaendelea na kulazimisha mashirika ya haki za binadamu kuchukua hatua. Zaidi ya hayo, Sheria ya Wahindi Asili wa Kanada ya mwaka 1876 ilitokana na ubaguzi.

Ugunduzi wa makaburi hayo ya umati kwa kweli ni ukumbusho wa ukweli kwamba tangu kuhama kwa Wazungu kutoka Ulaya kwenda bara Amerika Kaskazini, wenyeji wa Kanada wamekuwa wakibaguliwa rasmi na mchakato huo wa kikoloni ungali inaendelea.

Ingawa Waziri Mkuu wa Kanada Justin Trudeau amejaribu kuzipa uhuru wa kujitawala baadhi ya jamii za watu wa kiasili na kufidia kashfa iliyosababishwa na kufichuliwa kwa makaburi ya wanafunzi wa kiasili,lakini ukandamizaji na ubaguzi dhidi ya wenyeji wa Kanada umejikita katika historia ya nchi hiyo. Kwa hivyo kwa malipo ya fidia ya kimaonyesho na kipropaganda tu, Kanada, ambayo bado iko chini ya satwa ya Ufalme wa Uingereza, haiwezi kujivua lawama za ukandamizaji na mauaji ya kimbari ya wakazi asili wa nchi hiyo.

Perry Bellegarde mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wakanada Asili anasema kwamba kupatikana makaburi katika shule za zamani za bweni huko Kanada sio jambo jipya, na kubaini kuwa kadhia hiyo ni jeraha la zamani ambalo daima ni chungu kuliona.

Hayo yanajiri wakati ambao Kanada imekuwa ikijinadi kuwa mtetezi mkubwa wa haki za binadamu. Utawala wa Kanada umekuwa ukijitokeza katika katika majukwaa ya kimataifa kama vile Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa na kukosoa kile inachodai ni ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi zinazopinga ubeberu wa madola ya Magharibi.

Rekodi chafu ya haki za binadamu huko Kanada ni dosari kubwa kwa nchi hiyo ambayo ingali inaendelea kuwanyayasa wenyeji wa Kanada na kuwawekea kila aina ya vikwazo, kuwabagua na kuwashinikiza kwa njia mbalimbali.