Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

27 Januari 2023

15:09:20
1341425

Al-Azhar yatoa wito wa kususiwa bidhaa za Uswidi na Uholanzi

Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri kimetoa wito wa kususiwa bidhaa za Uswidi na Uholanzi ili kukabiliana na vitendo viovu vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika mataifa hayo ya Ulaya hivi karibuni.

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, Al-Azhar imetoa wito kwa Waislamu kote duniani hasa katika nchi za Kiarabu na Kiislamu "kususia bidhaa zote za Uholanzi na Uswidi na kuchukua msimamo thabiti na wa umoja wa kuunga mkono Qur’ani yetu Tukufu, Maandiko Matakatifu ya Waislamu. Hii itakuwa ni hatua muafaka  ya kutoa jibu kwa serikali za nchi hizi mbili, ambazo zimewaudhi Waislamu bilioni 1.5.”

Siku ya Jumapili, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi, na kiongozi wa kundi la chuki dhidi ya Uislamu la Pegida, alirarua kurasa za Qur’ani Tukufu  huko The Hague, mji mkuu wa Uholanzi. Video ya Wagensveld kwenye Twitter ilionyesha kuwa alichoma kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu.

Uchochezi huo mpya ulifuatia kitendo sawa na hicho cha chuki dhidi ya Uislamu siku ya Jumamosi nchini Uswidi, ambapo mtu mwenye msimamo mkali  raia wa Denmark alichoma nakala ya Qur’ani Tukufu mbele ya Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm, katika kitendo ambacho kiliidhinishwa na kusimamiwa na polisi nchini humo.

Taarifa ya Al Azhar imesema, "Wamevuka mipaka katika kulinda uhalifu wa kikatili na wa kinyama unaofanywa chini ya bendera maalumu ya kinyama na iliyo dhidi ya maadili ya kile kinachojulikana kama 'uhuru wa kujieleza'.

Al Azhar imetoa wito kwa Waarabu na Waislamu wote "kushikamana na kususia, na kuwaelimisha watoto, vijana na wanawake kuhusu hilo."

Aidha Al Azhar imesema, "Wapotovu hawa hawatathamini kamwe thamani ya dini - ambayo hawajui chochote kuihusu – na hawawezi kusitisha wanayoyafanya isipokuwa tu pale watakapokabiliana na changamoto za kifedha na kiuchumi. Hiyo ndiyo lugha pekee wanayoijua.”

Kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu kumezusha dhoruba ya lawama kutoka katika ulimwengu wa Kiislamu.

Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri kimetoa wito wa kususiwa bidhaa za Uswidi na Uholanzi ili kukabiliana na vitendo viovu vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika mataifa hayo ya Ulaya hivi karibuni.