Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

30 Januari 2023

17:01:46
1342389

Utawala wa Kizayuni umekiri kuhusu misaada yake ya nyuma ya pazia kwa Ukraine

Balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Ujerumani amekiri kuwa Tel Aviv inaisaidia pakubwa Ukraine katika vita dhidi ya Russia kuliko umma unavyofikiria.

Afisa huyo wa Kizayuni amekiri hilo katika hali ambayo nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, tangu miezi kadhaa iliyopita sambamba na kuongezeka mivutano katika vita huko Ukraine zinadai kuwa, Iran imeipatia Russia ndege zisizo na rubani (droni) na makombora ya balistiki ili kutumika katika vita dhidi ya Ukraine.  

Hossein Amir- Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu madai hayo ya Wamagharibi na kusema Iran iliipatia Russia droni chache kabla ya kuanza vita huko Ukraine. Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekanusha madai kwamba Tehran imetuma makombora kwa ajili ya Moscow. 

Shirika la habari la Sputnik limeripoti kuwa, Ron Prosor Balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mjini Berlin Ujerumani amekariri madai kwamba Iran imetuma silaha  Russia, Syria na Lebanon na kukiri kuwa Tel Aviv inaisaidia Ukraine nyuma ya pazia na kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko inavyoonekana mbele ya macho ya walimwengu. 

Balozi wa utawala wa Kizayuni nchini Ujerumani ameendelea kudai kuwa, moja ya sababu iliyoipelekea Tel Aviv kuchukua hatua kwa siri kuhusiana na vita vinavyoendelea huko Ukraine ni kutokana na kuwepo jamii ya Wayahudi huko Russia. 

Itakumbukuwa kuwa, Evgeny Kornichuk balozi wa Ukraine huko Tel Aviv aliwahi kusema kuwa, utawala wa Israel siku zijazo utaipatia Ukraine mifumo ya hali ya juu ya tahadhari dhidi ya ndege zisizo na rubani na makombora.

342/