Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

30 Januari 2023

17:02:19
1342390

Uturuki yawashauri raia wake wasiende Ulaya kutokana na hujuma zinazowalenga Waislamu

Uturuki imetoa onyo la kusafiri kwa raia wake wanaoishi au wanaopanga kwenda katika nchi za Ulaya, kutokana na chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za bara hilo.

Onyo hilo limetolewa baada ya maandamano ya mwishoni mwa juma lililopita nchini Uswidi ambapo mwanaharakati anayepiga vita Uislamu alichoma moto nakala ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani mbele ya Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm, katika kitendo ambacho kiliidhinishwa na kusimamiwa na polisi wa Sweden.

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Uturuki imewataka raia wa nchi hiyo kuchukua tahadhari na kujiepusha na maeneo ya maandamano katika nchi za Ulaya. Pia imesema wanapaswa kwenda kwa mamlaka za mitaa ikiwa watakabiliwa na mashambulizi ya chuki au ubaguzi.

Uturuki ni miongoni mwa nchi za Kiislamu zilizolaani vikali kitendo cha mwanaharakati wa siasa kali za mrengo wa kulia, Rasmus Paludan, cha kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu katika mji wa Stockholm, ambacho alikikariri tena Ijumaa mjini Copenhagen. Ankara pia ilimwita na kumsaili balozi wa Uholanzi baada ya mwanaharakati mwingine wa siasa kali za mrengo wa kulia kurarua kurasa za kitabu kitakatifu cha Qura'ni huko The Hague.

Kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu kumezusha wimbi la hasira na malalamiko makali ya Waislamu kote duniani, na watetezi wa uhuru wa itikadi pia wamelaani vikali kuchomwa moto nakala ya kitabu hicho kitakatifu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Misri, Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu, taasisi ya Al-Azhar nchini Misri, Baraza la Wanazuoni wa Kiislamu Duniani, Qatar, Saudi Arabia, Indonesia, Jordan, Morocco, Mauritania, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Hamas na harakati ya Jihad ya Kiislamu ya Palestina ni miongoni mwa nchi na taasisi zilizochukua msimamo mkali dhidi ya kitendo hicho cha kuchukiza na kutoa wito wa kuadhibiwa wahusika.

Ijumaa ya wiki hii pia mamilioni ya Waislamu wa Iran walifanya maandamana baada ya Swala ya Ijumaa kote nchini wakilaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya.

Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri kimetoa wito wa kususiwa bidhaa za Uswidi na Uholanzi ili kukabiliana na vitendo viovu vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika mataifa hayo ya Ulaya hivi karibuni.

342/