Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Februari 2023

12:22:22
1343300

Moscow yakosoa kimya cha nchi za Ulaya kuhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

Mwenyekiti wa Baraza la Shirikisho la Urusi (Bunge la Federesheni ya Russia) ametoa wito kwa mabunge ya Ulaya kulaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za bara hilo.

Valentina Matviyenko ametoa wito kwa mabunge ya Ulaya kulaani vikali vitendo hivyo viovu na kuchukua hatua zote muhimu kuzuia kukaririwa kwake.

Mwenyekiti wa Baraza la Shirikisho la Urusi amesisitiza kuwa, kuvunjia heshima matakatifu ni jinai na uhalifu unayozidisha chuki baina ya watu na kuongeza kuwa: Serikali zote zenye akili timamu duniani zinapaswa kulaani vitendo hivyo na kuvikomesha.

Akilaani kuchomwa moto nakala ya Qur'ani mbele ya ubalozi wa Russia nchini Denmark, Valentina Matviyenko amesema: Mabalozi wa nchi zinazoruhusu vitendo hivyo waitwe na kusailiwa.

Matamshi hayo yanafuatia hatua ya baadhi ya wanasiasa wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia katika nchi za Ulaya kuchoma moto na kurarua nakala za kitabu kitakatifu cha Qur'ani chini ya usimamizi wa serikali za nchi hizo.

Kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu kumezusha wimbi la hasira na malalamiko makali ya Waislamu kote duniani, na watetezi wa uhuru wa itikadi pia wamelaani vikali kuchomwa moto nakala ya kitabu hicho kitakatifu.

Ijumaa iliyopita pia mamilioni ya Waislamu wa Iran walifanya maandamana baada ya Swala ya Ijumaa kote nchini wakilaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya. 

342/