Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

4 Februari 2023

11:35:58
1343517

Iran yatoa mwito wa kupanuliwa uhusiano wake na Venezuela

Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Venezuela wametilia mkazo udharura wa kuzidisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti bila vizingiti.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye yuko katika ziara rasmi ya kikazi jijini Caracas ametoa mwito wa kuimarisha zaidi ushirikiano wa Iran na Venezuela katika nyuga zote ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika kupambana na ubeberu wa Marekani.

Hapo jana, Amir-Abdollahian alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Nocolas Maduro wa Venezuela, ambapo walijadili umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hizi, mbali na kugusia pia masuala ya kieneo na kimataifa.

Uhusiano wa Venezuela na Iran ni wa muda mrefu, wa zaidi ya karne moja nyuma. Hivi sasa pia nchi hizi mbili kwa pamoja ziko chini ya mashinikizo na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani.

Kuhusu vikwazo hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Tehran na Caracas zinapaswa kuwa na jitihada za pamoja, na kutekeleza makubaliano baina ya nchi mbili hizi, ili ziweze kuondokana na athari za mashinikizo hayo ya madola la kibeberu.

Kabla ya kukutana na Rais Maduro, Amir-Abdollahian alikutana na mwenzake wa Venezuela, Yvan Gil Pinto, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili vita vya Ukraine.

Abdollahian ambaye aliwasili Caracas siku ya Alkhamisi ameeleza bayana kuwa, "baadhi ya madola yanatumia kadhia ya haki za binadamu kwa ajili ya kuzishinikiza kisiasa nchi nyingine."

Kwa upande wake, Yvan Gil Pinto, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema Iran na nchi hiyo ya Amerika Kusini ni washirika wakuu katika kupambana na vikwazo na mashinikizo ya mabeberu katika miaka ya karibuni.

Amepongeza ushirikiano wa mataifa haya mawili katika fremu ya Kundi la Marafiki wa Kuihami Hati ya Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, jitihada zaidi zinahitajika katika uga huo.

342/