Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

4 Februari 2023

11:36:50
1343519

Al-Nahdha: Kususiwa uchaguzi ni risala ya wazi ya wananchi wa Tunisia kwa utawala wa Kais Saied

Harakati ya al-Nahdha ya Tunisia imetangaza kuwa, hatua ya wananchi wengi wa nchi hiyo ya kususia uchaguzi na kutojitokeza katika duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge uliofanyika hivi karibuni ni ujumbe wao wa wazi kabisa wa kutaka kuhitimishwa mapinduzi ya Rais Kais Saied.

Taarifa ya harakati hiyo ambayo ni mrengo mkuubwa zaidi wa upinzani nchini Tunisia imesisitiza kuwa, Rais Kais Saied anapaswa kutambua kwamba, huu ndio msimamo wa wananchi waliowengi wa nchi hiyo kuhusiana na utawala wake pamoja na hatua alizochukua.

Jumapili iliyopita wapiga kura nchini Tunisia walielekea katika vituo vya kupigia kura kushiriki awamu ya pili ya uchaguzi wa bunge huku kukiwa na mzozo mkubwa wa kisiasa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Idadi ya waliojitokeza katika duru ya pili ya uchaguzi mkuu wa kabla ya wakati wake, uliofanyika  ni asilimia 11.3 tu.

Ikumbukwe kuwa, akthari ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura nchini Tunisia walisusia pia duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge uliofanyika Disemba 17 mwaka uliopita 2022. 

Mnamo Julai 25, 2021, Rais Kais Saeid, alipitisha maamuzi na kuchukua hatua kadhaa zisizo za kawaida ikiwemo kutangaza kufuta mamlaka ya Bunge, kuondolewa kwa kinga ya Wabunge, kumfuta kazi Waziri Mkuu na kuvunja tume ya usimamizi wa katiba, hatua ambazo zilizusha mtafaruku na mkwamo wa kisiasa nchini Tunisia, ambao uliambatana na wimbi la maandamano ya vyama na mirengo ya kisiasa, kikiwemo chama cha Kiislamu cha al-Nahdha.

Maamuzi ya Rais wa Tunisia yameendelea kupingwa na kulalamikiwa na vyama na asasai mbalimbali na kuifanya nchi hiyo iendelee kushuhudia mzozo wa kisiasa na kijamii huku uchumi wake ukizidi kuzorota.

342/