Main Title

source : Parstoday
Jumapili

5 Februari 2023

16:07:22
1343820

Watu 14 wapoteza maisha katika ajali ya barabarani nchini Kenya

Watu wasiopungua 14 wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika barabara ya Lodwar- Kakuma eneo la Kakwamunyen, kaunti ya Turkana, kaskazini magharibi mwa Kenya.

Kamanda wa Polisi katika kaunti ndogo ya Turkana ya Kati, Lemmy Njiru amesema waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni wanawake wanane, wanaume watatu na watoto wavulana watatu. Aidha watu 13 wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo.

Amesema ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa lori lililokuwa limejaa abiria na mizigo kupita kiasi kubingiria likijaribu kukwepa kugonga ngamia aliyekuwa akivuka barabara katika eneo hilo la Kakwamunyen.

Njiru amesema majeruhi wanatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ndogo ya Lodwar, huku miili ikipelekwa katika hifadhi ya maiti katika eneo hilo. Malori ndiyo hutumika zaidi kuwasafirisha abiria na mizigo katika kaunti ya Turkana.

Ajali za barabarani limekuwa janga la muda mrefu nchini Kenya, ambapo kwa wastani nchi hiyo husajili vifo 3,000 vya ajali kwa mwaka.

Katika hatua nyingine, idadi ya watu waliofariki dunia kwenye ajali iliyotokea wilayani Korogwe mkoani Tanga nchini Tanzania ikihusisha gari la mizigo ‘Fuso’ na Coaster imefikia 20 baada ya majeruhi wengine wawili kufariki dunia leo. Taarifa ya kuongezeka idadi ya marehemu hao imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba kwenye ibada ya kuaga miili hiyo iliyofanyika Hospitali ya Magunga wilayani Korogwe.

Kati ya wahanga wawili wa ajali hiyo, mmoja alikuwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo na mwingine Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam. Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana Jumamosi Februari 4,  wakati wakisafirisha mwili kwenda kuzikwa mkoani Kilimanjaro, ambapo 18 walifariki papo hapo.

Ongezeko la ajali za barabarani katika nchi hizo Afrika Mashariki linatajwa kusababishwa na uzembe, madereva kutoheshimu sheria za barabarani, barabara mbovu zenye mashimo na miembamba, magari mabovu na kujaza abiria na mizigo kupita kiasi. 

342/