Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

6 Februari 2023

16:07:44
1344090

Wananchi wa Sudan waandamana kupinga uhusiano na Israel

Wananchi wa Sudan waliandamana katika mji mkuu Khartoum siku ya Jumapili kupinga hatua ya utawala wa kijeshi nchini humo kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala haramu wa Israel Eli Cohen alitembelea Sudan ambapo alikutana na mkuu wa jeshi na kiongozi wa nchi hiyo,  Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.

Cohen alisema kuwa utawala wa Israel na Sudan zimekamilisha maandishi ya makubaliano ya amani ambayo yatatiwa saini "baadaye mwaka huu."

Waandamanaji waliokusanyika katikati mwa Khartoum walipeperusha mabango ya kulaani kuhalalisha uhusiano kati ya Sudan na Israel.

Miongoni mwa mabango yaliyopeperushwa na waandamanaji yalikuwa yana maandishi kama vile "Palestina haiuzwi" na "Khartoum haitasaliti Al Quds (Jerusalem)" .

Hayo yanajiri baada ya vyama na makundi ya kisiasa ya Sudan kutangaza msimamo kuhusiana na safari ya hivi karibuni ya waziri wa mambo ya nje wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel nchini humo kwa kusisitiza kuwa yataendelea kulihami na kuliunga mkono taifa la Palestina na mapambano yake matukufu.

Katika msimamo rasmi viliotoa kuhusiana na safari ya waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni mjini Khartoum, vyama na asasi hizo za Sudan zimetangaza kuwa kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni hakukubaliki kwa sababu hakuendani na maadili na imani za Kiislamu za taifa la Sudan.

Al-Burhan, mkuu wa Baraza Kuu la Utawala la Sudan, aliwahi kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mwezi Februari 2020 katika mji wa Entebbe nchini Uganda.

Sudan itakuwa nchi ya sita ya Kiarabu kuanzisha uhusiano na Israel.

Misri ilitia saini mkataba wa amani na Israel mwaka 1979, ikifuatiwa na Jordan mwaka 1994. Na mwaka 2020, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain na Morocco pia zilitangaza mikataba ya kurejesha uhusiano na Israel.

342/