Main Title

source : Parstoday
Jumanne

7 Februari 2023

16:41:25
1344430

Katibu Mkuu wa UN: Dunia inaelekea katika vita vikubwa zaidi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kwamba, hatua zozote za kuchochea mgogoro wa Russia na Ukraine huenda zikaitumbukiza dunia katika vita vipana na vikubwa zaidi.

Antonio Guterres, alitoa indhari hiyo jana Jumatatu katika hotuba yake mbele ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, ulimwengu unakaribia kutumbukia katika vita vikubwa zaidi.

Guterres ameeleza kuwa, "Jamii ya kimataifa si tu inatembea (taratibu) ndotoni ikielekea katika vita vikubwa zaidi, lakini inaelekea kwa upesi kwenye vita hivyo. Matumaini ya amani yanazidi kufifia, huku nafasi ya kupanua zaidi mgogoro na umwagaji damu ikiendelea kuwa kubwa zaidi."

Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, mazungumzo, mashauriano na diplomasia ni nyenzo na njia bora zaidi za kufikia ulimwengu bora na wenye amani.

Guterres amebainisha kuwa, changamoto za kimataifa za kipindi kilichopita bado zingalipo, na mchakato wa kuimarisha amani na maendeleo endelevu uko hatarini. Amesema, 'Iwapo kila nchi itafungamana na wajibu wake kwa mujibu wa Hati ya UN, haki ya amani itadhaminiwa."

Kauli ya Katibu Mkuu wa UN inakuja katika hali ambayo, serikali ya Moscow imeonya mara kadhaa kwamba, uamuzi wa Wamagharibi wa kurundika silaha za kila aina huko Ukraine utajibiwa vikali na Russia.

Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika hotuba yake hiyo mbele ya Baraza Kuu la UN amegusia juu ya taathira hasi za mabadiliko ya tabianchi kwa ulimwengu, na mgogoro wa umaskini na uchochole unaoisumbua dunia na kusisitiza kuwa, kuna hata kwa serikali za dunia kuchukua hatua za dharura za kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo.

342/