Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

9 Februari 2023

15:22:25
1344999

Venezuela yaonyesha mshikamano wake kwa Uturuki na Syria; yatuma misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa zilzala

Kikosi cha waokoaji 52 wa Venezuela na wahudumu wa idara ya zima moto waliondoka jana Jumatano Caracas wakielekea katika nchi za Uturuki na Syria kwa ajili ya operesheni ya uokoaji wa waathirika wa tetemeko la ardhi lililozikumba nchi hizo.

Serikali ya Venezuela mbali na kutuma tani 22 za misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa Uturuki na Syria ambazo zimekumbwa na mtetemeko mkubwa wa ardhi, imetuma pia timu za waokoaji na wataalamu kushiriki katika shughuli za uokoaji katika maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi katika nchi mbili hizo. 

Venezuela imetuma Uturuki na Syria tani 22 za misaada ya kibinadamu na mbwa sita wa uokoaji kupitia shirika la ndege la serikali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ndege hiyo kutoka Venezuela imepangwa kutua kwanza huko Syria na baada ya kupakua baadhi ya misaada ya chakula dawa ndege hiyo itlitazamiwa kuelekea nchini Uturuki.  

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amemwakilisha Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro ambapo alifika katika uwanja wa ndege mjini Caracas wakati wa kupakiwa shehena hiyo ya misaada na kwa mara nyingine tena akatangaza mshikamamo wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini na watu wa Uturuki na Syria. Amesisitiza kuwa, wakati umefika kwa jamii ya kimataifa kupaza sauti zao ili kuindolea Syria vikwazo na kutoa mwanya kwa nchi hiyo kujidhaminia mahitaji yake. 

Venezuela imetoa misaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi huko Uturuki na Syria huku nchi hiyo yenyewe ikikabiliwa na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani.

Tetemeko la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha Rishta Jumatatu wiki hii liliyakumba maeneo ya kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria. Hadi sasa maelfu ya watu wameuliwa na wengi wengi kujeruhiwa katika zilzala hiyo kubwa. Maafisa husika wa Uturuki wametangaza kuwa watu walipoteza maisha hadi sasa ni zaidi ya elfu 12 na mia tatu na majeruhi ni zaidi ya elfu 60.

Nchini Syria pia zaidi ya watu 2500 wameripotiiwa kufariki dunia hadi sasa kutokana na tetemeko hilo huku juhudi za kutafuta manusura zikiendelea 

342/