Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

10 Februari 2023

20:41:11
1345308

Spika wa Bunge la Russia: Rais Biden wa Marekani ni "gaidi" kwa kuamuru Nord Stream iripuliwe

Spika wa Bunge la Russia Vyacheslav Volodin amesema, Rais Joe Biden wa Marekani ni gaidi kutokana na kutoa amri ya kutekelezwa hujuma ya kubomoa muundombinu wa nishati barani Ulaya.

Volodin amemtaja rais wa Marekani Joe Biden kuwa "gaidi" baada ya ripoti ya mwandishi wa habari mashuhuri wa ripoti za uchunguzi wa Marekani Seymour Hersh kuilaumu Washington kwamaba ilihusika na hujuma dhidi ya mabomba ya gesi ya Nord Stream iliyotokea mwaka jana.

Katika ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa Telegram, Spika huyo wa Duma la Russia amesema: "hotuba kuu kwa taifa aliyotoa Biden, ambayo  alidai ndani yake kwamba Marekani ni "taifa linalosimama kama mwanga unaoangazia ulimwengu" imemkumbusha "kauli za viongozi wa utawala wa Kinazi wa Ujerumani".

Mnamo siku ya Jumatano, ripota mchunguzi wa Marekani Seymour Hersh alitoa ripoti yake ya uchunguzi aliofanya, akiishutumu serikali ya Washington kuwa ndiyo iliyohusika na miripuko iliyotokea Septemba mwaka jana kwenye mabomba ya usafirishaji gesi ya Nord Stream. 

Kulingana na chanzo cha habari cha kuaminika kilichozungumza na Hersh, mada za miripuko ziliwekwa kwenye mabomba makuu katika Bahari ya Baltic mnamo Juni 2022 na wazamiaji wa Jeshi la Marekani kwa kutumia kivuli cha mazoezi ya kijeshi ya shirika la kijeshi NATO na kisha yakaripuliwa baadaye kwa kutumia rimoti kutokea mbali.

Spika wa bunge la Russia amebainisha kuwa, kama aliyekuwa rais wa Marekani Harry Truman alikuwa mhalifu kwa kutumia silaha za nyuklia dhidi ya raia huko Hiroshima na Nagasaki, basi Biden ni gaidi, ambaye ameamuru hujuma dhidi ya miundombinu ya nishati ya washirika wake wa kimkakati, ambao ni Ujerumani, Ufaransa na Uholanzi.

Volodin amesisitiza kuwa, ufichuaji uliofanywa na Hersh inapasa uwe msingi wa uchunguzi wa kimataifa wa "kumfikisha Biden na washirika wake mbele ya sheria," na kuhakikisha kuwa mataifa yaliyoathiriwa na "shambulio hilo la kigaidi" yanalipwa fidia.

Mabomba ya Nord Stream 1 na 2 yamekuwa njia muhimu za usambazaji gesi ya Russia kuelekea Ulaya kupitia Ujerumani.../

342/