Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

17 Februari 2023

20:36:09
1347081

UN yawasilisha ombi la msaada wa dola bilioni moja kusaidia waathirika wa Zilzala Uturuki

Umoja wa Mataifa umezindua ombi la dola bilioni moja kwa ajili ya usaizidi wa kibinadamu kwa wananchi wa Uturuki wanaokumbwa na machungu kufuatia tetemeko kubwa zaidi la ardhi kuwahi kukumba taifa hilo katika kipindi cha karne.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema fedha hizo zitakazotumika kwa kipindi cha miezi mitatu zitasaidia watu milioni tano na laki mbili na kuwezesha mashirika ya misaada kuimarisha kasi ya usaidizi wao kwa juhudi za serikali za kupeleka misaada kwenye maeneo kadhaa ikiwemo misaada ya chakula, ulinzi, elimu, maji na malazi.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa katika makao makuu ya umoja huo jijini New York, imemnukuu Katibu Mkuu Guterres akisema “Uturuki ni nyumbani kwa wakimbizi wengi zaidi duniani na kwa miaka mingi imekuwa ikionesha ukarimu wa kipekee kwa majirani zao Syria. Sasa ni wakati wa dunia kusaidia wananchi wa Uturuki kama vile ambavyo wamekuwa wakishikamana na wengine wanaosaka misaada.”

Katika wito huo kwa jamii ya kimataifa Katibu Mkuu wa UN ameendelea kusema: “mahitaji ni makubwa, watu wanapitia machungu na hakuna muda wa kupoteza. Nasihi jamii ya kimataifa iongeze juhudi na kufadhili kwa ukamilifu ombi hili ili kupatia jawabu janga kubwa zaidi la kimaumbile kuwahi kutokea katika zama zetu.”

Wakati huohuo Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura OCHA imesema majengo 47,000 yameporomoka au kubomoka kiasi, na maelfu ya watu wamesaka hifadhi katika makazi ya muda nchini kote Uturuki.

Shule, hospitali na huduma nyingine za msingi zimevurugwa au kuharibiwa kabisa na tetemeko hilo laardhi huku familia nyingi zikiwa zimetenganishwa, mamia ya watoto wamebakia yatima au hawawezi kuunganishwa na wazazi wao.

OCHA imesema, kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Uturuki, zaidi ya watu milioni tisa wameathiriwa na tetemeko hilo la ardhi nchini huumo na hadi tarehe 15 mwezi huu wa Februari, zaidi ya watu 35,000 wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na tetemeko hilo.

Tetemeko la ardhi lililopiga Uturuki na Syria Jumatatu ya tarehe 6 Februari, limetokea wakati wa kilele cha majira ya baridi kali, na kuacha mamia ya maelfu ya watu wakiwemo watoto na wazee bila fursa ya malazi, chakula, maji, vipasha joto na huduma za afya.../


342/