Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

17 Februari 2023

20:36:36
1347082

Mpigano, majanga ya tabianchi na ukimbizi vinawakosesha masomo watoto milioni 78 duniani

Watoto wa kike na wa kiume milioni 78 duniani kote hawaendi skuli kabisa kutokana na mapigano, mizozo, majanga ya tabianchi na ukimbizi ilhali wengine makumi ya mamilioni wanapata elimu ya hapa na pale. Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Akihutubia kwa njia ya video mkutano wa kusaka dola milioni 222 kusaidia elimu kwa watoto walio kwenye majanga na mizozo ulioandaliwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kufikisha elimu kwenye maeneo ya majanga na mizozo ya muda mrefu, uitwao Education Cannot Wait au Elimu Haiwezi Kusubiri, ambao unafanyika mjini Geneva, Uswisi Guterres amesema hakuna mtu anapaswa kunyimwa fursa ya kujifunza. 

Amesema kwa ujumla watoto milioni 222 leo hii wanapata elimu isiyo na umakini. 

“Haijalishi uko wapi, haijalishi unaishi wapi na wala vikwazo unavyokumbana navyo, ni lazima upate elimu bora,” amesema Katibu Mkuu wa UN akitoa wito wa juhudi zaidi za kimataifa kuhakikisha watoto wengi zaidi walio hatarini na wengineo wanapata fursa ya kufanikiwa. 

Katibu Mkuu wa UN amekaribisha suala kwamba tangu ulipoanzishwa mfuko wa Elimu Haiwezi Kusubiri mwaka 2017 walimu 87,000 wamepatiwa mafunzo na kuwapatia watoto milioni saba wanaoishi kwenye maeneo ya majanga elimu wanayostahili.

 Wakati ahadi kutoka nchi 18 na sekta binafsi zimefikia milioni 826 katika siku ya kwanza ya mkutano huo ulioanza jana, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu Duniani na pia Mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu la ECW, Gordon Brown amekaribisha usaidizi wa kimataifa juu ya fursa ya kusoma kwa wote akisema ni uwekezaji wa amani endelevu. 

Naye Neema Lugangira, mbunge kutoka nchini Tanzania ambaye pia ni mwakilishi wa Afrika katika mtandao wa wabunge vinara wa elimu duniani amesisitiza kuwa, fedha zinazochangishwa katika mkutano huo zipelekwe pia kwa nchi zinazopokea wakimbizi ili ziweze kutoa huduma inayotakiwa.../


342/