Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

20 Februari 2023

16:25:48
1347744

Guterres: Afrika ipewe kiti cha kudumu Baraza la Usalama la UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameunga mkono wito wa kutolewa kiti cha kudumu cha Baraza la Usalama kwa bara la Afrika.

Antonio Guterres ameyasema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa viongozi wa Afrika uliomalizika jana mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia.

Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar imemnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, akisema katika Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Afrika huko Addis Ababa, kuwa mabadiliko ya muundo wa Baraza la Usalama ni muhimu ili kuruhusu ushiriki wa kiadilifu wa nchi za Afrika. 

Antonio Guterres amesema kuwa Umoja wa Afrika umechukua hatua kubwa za kustawisha nchi za bara hilo, na Umoja wa Mataifa unakaribisha juhudi za kuanzisha eneo huria la biashara barani Afrika.

Awali Moussa Faki, mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alitangaza katika hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi za Afrika mjini Addis Ababa, kwamba bara la Afrika linapaswa kuwa na mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama.

Itakumbukwa kuwa, wakati wa mazungumzo ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama mnamo Novemba 2022, wawakilishi wa Afrika walitoa wito wa kupanuliwa zaidi taasisi hiyo na uwepo wa Afrika kati ya wanachama wa kudumu na wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama. 


342/