Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

20 Februari 2023

16:50:44
1347753

Mauritius yanyemelewa na kimbunga cha Freddy; yasimamisha safari za ndege

Mauritius imesimamisha safari za ndege na kufunga soko lake la hisa huku kimbunga cha Freddy kikiinyemelea nchi hiyo na hivyo kuwa tishio kwa kisiwa hicho kilichoko katika bahari ya Hindi.

Upepo mkali wa kasi ya kilomita 120 kwa saa umerekodiwa huko Mauritius hii leo. Mauritius na nchi nyingine zinazopatikana katika bahari ya Hindi kama Madagascar na Msumbiji mara kwa mara zimekuwa zikiathiriwa na tufani na vimbunga vikali vyenye nguvu ya kubomoa nyumba, miundo mbinu na kuharibu mazao ya kilimo. 

Kisiwa cha Mauritius kinajulikana kwa kuwa na maeneo mengi mazuri ya kuvutia ya kupumzikia ikiwa ni pamoja na fukwe za  mchanga mweupe n.k. idara ya Hali ya Hewa ya nchi hiyo imeripoti kuwa, kimbunga hicho leo mchana kimepita katika umbali wa kilomita 120 kwa sasa kuelekea maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo huku kikiashiria tishio la moja kwa moja. Idara hiyo imewataadhirisha watu kutoelekea katika maeneo ya baharini ili kuepuka kudhurika na kimbunga hicho.  Huku haya yakiripotiwa, maafisa husika katika kisiwa cha Madagascar ambacho pia kinapatikana katika bahari ya Hindi wamesema kuwa mvua kubwa zinatarajia kunyesha hadi kufikia kesho jioni katika maeneo ya Mahanoro mashariki mwa nchi hiyo na Manakara kusini mashariki mwa nchi. Mvua hizo zinatarajiwa kusababisha mafuriko katika maeneo ya pwani ya Madagascar ambapo Ofisi ya Idara ya Kupambana na Majanga ya Madagascar tayari imetuma mahema, kamba na vifaa vingine muhimu katika wilaya nne ambazo zinatazamiwa kuathiriwa pakubwa na mafuriko. Mwezi Januari mwaka huu kimbunga cha kitropiki kwa jina la "Cheneso" kiliuwa watu 33 huko Madagascar. 

342/