Main Title

source : Parstoday
Jumanne

21 Februari 2023

18:37:12
1348035

Ujerumani: Hatuna misingi ya sheria ya kuiweka IRGC katika orodha ya ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani ameashiria hatua ya Bunge la Ulaya ya kupiga kura ya kuongeza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika orodha ya makundi ya 'kigaidi' ya Umoja wa Ulaya na kusisitiza kuwa, hakuna misingi ya sheria ya kuiwepa SEPAH kwenye faharasa hiyo.

Akizungumza jana Jumatatu katika kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa EU mjini Brussels, Annalena Baerbock, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ujerumani alisema, "Kwa sasa, hatuna mashiko ya kisheria ndani ya EU ya kuongeza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika orodha ya makundi ya kigaidi."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Ujerumani amebainisha kuwa, wataalamu wa nchi hiyo ya Ulaya hawajaweza kupata misingi yoyote ya kisheria ya kuweza kuhalalisha hatua hiyo dhidi ya SEPAH ya Iran, kauli ambayo inashabihiana na iliyotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Sera za Nje wa EU, Josep Borrell.

Mwezi uliopita, Bunge la Umoja wa Ulaya lilipitisha marekebisho ambayo yaliongezwa kwenye ripoti ya kila mwaka ya sera ya mambo ya nje na kutaka nchi wanachama wake kuijumuisha IRGC katika orodha yao ya magaidi.

Bunge hilo pia lilipitisha azimio jingine likitaka vikwazo zaidi dhidi ya watu binafsi na mashirika ya Iran na kuiweka IRGC katika orodha ya magaidi wa Umoja wa Ulaya kutokana na madai ya ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa ghasia za hivi majuzi.

Viongozi wa Iran walilaani vikali kitendo hicho. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliashiria hatua hiyo ya Bunge la Ulaya dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kueleza kuwa, jeshi la IRGC limekabiliana na magaidi na kuzima shari za magaidi katika eneo la Asia Magharibi.

Ujerumani imetoa kauli hiyo ya kujikanganya katika hali ambayo, Umoja wa Ulaya umetangaza vikwazo vipya dhidi ya shakhsia 32 na taasisi mbili za Jamhuri ya Kiislamu, wakiwemo maafisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

342/