Main Title

source : Parstoday
Jumatano

22 Februari 2023

17:56:18
1348318

CNN: Ni asilimia 5.7 tu ya madaktari wa Marekani ndio wenye asili ya Afrika; wataalamu wanaonya

Wataalamu wameonya kuhusu idadi ndogo ya madaktari wenye asili ya Afrika walioko nchini Marekani ikilinganishwa na idadi jumla ya Wamarekani hao.

Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Muungano wa Vyuo vya Tiba vya Marekani zinaoenesha kuwa, Wamarekani wenye asili ya Afrika wanaunda takriban asilimia 5.7 tu ya madaktari wote nchini Marekani.

Takwimu hizo lakini hazikusema madaktari hao wanahudumia jamii gani hasa. Inakadiriwa kwamba, Wamarekani wenye asili ya Afrika wanaunda asilimia 12 ya Wamarekani wote.

Michael Dill, mkurugenzi wa tafiti za nguvu-kazi wa Chama cha Vyuo vya Udaktari vya Marekani anasema, moja ya sababu zinazoweza kutolewa kuhusu asilimia ndogo ya madaktari weusi nchini Marekani ikilinganishwa na idadi yao ni kubaguliwa na kutengwa kihistoria watu weusi kwenye masuala ya tiba. Amesema, ubaguzi wa rangi wa kitaasisi umekita mizizi katika jamii ya Marekani.Vyuo vingi vya matibabu vya Marekani vina historia ya kutokubali wanafunzi wasio wazungu. Mmarekani wa kwanza mweusi kupata shahada ya matibabu, Dk James McKeon Smith, alilazimika kujiunga na Chuo Kikuu cha Glasgow School of Medicine nchini Scotland na kuchukulia huko shahada yake. Dk Smith alipata udaktari wake mwaka wa 1837, akarudi New York Marekani, akawa Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Afrika kuendesha duka la dawa nchini Marekani, na alikuwa na makala zilizochapishwa katika majarida ya matibabu ya nchi hiyo. Miongo michache baadaye, mwaka wa 1900, kulingana na utafiti, asilimia 1.3 ya madaktari walikuwa Wamarekani wenye asili ya Afrika. Katika kipindi cha zaidi ya miongo minne kati ya 1978 na 2019, idadi ya waliojiandikisha katika vyuo vya matibabu vinavyojumuisha watu wenye asili ya Afrika, Walatino na jamii nyingine za watu wachache ilikuwa ndogo sana ikilinganishwa idadi ya wananchi wote wa Marekani. Sasa Marekani inachunguza historia yake ya ubaguzi wa rangi katika masuala ya tiba na matibabu.