Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

27 Februari 2023

16:36:50
1349485

Onyo kali la Korea Kaskazini kwa Marekani

Korea Kaskazini imetoa onyo kali kwa Marekani na kusema kuwa kuendelea vitendo vya kichochezi vya Marekani kunaweza kuhesabiwa kuwa ni kutangaza vita dhidi ya Pyongyang.

Onyo hilo kali la Korea Kaskazini limetolewa baada ya Marekani na Korea Kusini kufanya luteka na mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika maji ya karibu na Korea Kaskazini na hivyo kuwatia wasiwasi viongozi wa Pyongyang. Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Marekani cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini amesema kuwa, njia pekee ya kuzuia kuwa mbaya zaidi hali ya mambo na mizozo ya kijeshi katika peninsula ya Korea na maeneo ya karibu yake ni Marekani kukomesha siasa zake za kibeberu na kutopeleka zana zake za kimkakati huko Korea Kusini. Vile vile iache siasa zake za kichochezi za kufanya mazoezi ya mara kwa mara ya kijeshi katika maeneo ya karibu na Korea Kaskazini. Tab'an ni jambo lililo wazi kabisa kwamba Marekani haiwezi kukubaliana na mwito huo na itaendelea na siasa zake za kiistikbari kwa kushirikiana na Korea Kusini na Japan. 

Ji Nak Yung, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anazungumzia suala hilo akisema: Inachofanya Marekani katika kisiwa cha Korea na maeneo ya karibu yake, ni kuchochea machafuko na ukosefu wa amani tu. Huo ndio wenzo unaotumiwa na Washington kujaribu kufanikishia siasa zake za kueneza chuki dhidi ya Korea Kaskazini. Hii ni katika hali ambayo Korea mbili, mara kwa mara zimeonesha nia ya kuweka pembeni tofauti zao na kuishi pamoja kwa usalama na amani, lakini hilo linakinzana kikamilifu na siasa za kiistikbari za Marekani.

Kwa mtazamo wa Korea Kaskazini, taasisi za kimataifa zenye ushawishi katika masuala ya usalama duniani likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hazipaswi kunyamazia kimya uchochozi huo wa Marekani. Pyongyang inaamini kuwa, misimamo ya wazi ya wanachama wa Baraza la Usalama ina nguvu za kukabiliana na siasa za kichochezi na kibeberu za Marekani. Aidha viongozi wa Korea Kaskazini wanaamini kuwa, kimya cha Umoja wa Mataifa kinaongeza kiburi cha Marekani na kuzidisha mashinikio kwa Prongyang. Ni kwa sababu hiyo ndio maana mara kwa mara Korea Kaskazini ikawa inasisitiza kwamba kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linazo nguvu za kuepusha mivutano katika kisiwa cha Korea, lakini kama kweli lina nia ya kufanya hivyo.  

Hii ni kwa sababu mara kwa mara Marekani inalitumia Baraza la Usalama kutoa maazimio dhidi ya nchi zisizokubali kuburuzwa na Washington. Soroush Amiri, mtaalamu mwingine wa masuala ya kimataifa anasema: Siasa za Marekani ni kuzidhoofisha nchi zinazoipinga kwa kutumia vikwazo na kutoa maazimio kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuzizuia nchi zinazopinga siasa za Marekani zisiweze kujihami na kujitetea. Ni kwa sababu hiyo ndio maana mara kwa mara Korea Kaskazini inaulaumu Umoja wa Mataifa kwa kukubali kutumiwa vibaya na Marekani na imekuwa mara nyingi ikilitaka Baraza la Usalama lichukue hatua madhubuti za kukabiliana na siasa za kibeberu za Washington.

Alaakullihaal, kwa mtazamo wa Korea Kaskazini, kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina nia ya kweli ya kuleta amani duniani, likiwemo eneo la Korea, basi linapaswa kuilazimisha Marekani na Korea Kusini kukomesha siasa zao za kujirundikia silaha na kufanya luteka za kijeshi karibu na maeneo ya Korea Kaskazini. Lakini inaonekana wazi kwamba Japan na Korea Kusini zitaendelea kukubali kuwa nyenzo za Marekani za kuishinikiza Korea Kaskazini na matokeo ya siasa hizo mbovu si mengine ghairi ya kuzidisha hali ya wasiwasi na kuhatarisha usalama wa dunia nzima.

342/