Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Machi 2023

13:50:48
1350200

Umoja wa Mataifa waanzisha uchunguzi katika mauaji ya watu wa asili wa Kanada

Kufichuliwa mauaji ya wakazi asilia wa Kanada, hasa watoto, kumeibua kashfa kubwa dhidi ya nchi hiyo inayodai kuwa mtetezi wa haki za binadamu ulimwenguni. Kuhusiana na hilo, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuanza shughuli yake ya uchunguzi kuhusu mauaji hayo ya kimbari ya watu asilia wa Kanada.

Uchunguzi huo umeanzishwa na Cali Tzay, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za watu asilia. Tzay anatoka nchini Guatemala na katika mojawapo ya makabila asilia ya nchi hiyo ya Amerika ya Kati.

Akizungumzia jambo hilo, Kenneth Deer, mkuu wa shirikisho la jumuiya tano za kiasili nchini Kanada, anasema kuwa picha zinazoonyeshwa nje ya mipaka ya Kanada zinaonyesha kwamba kila kitu katika nchi hiyo ni shwari kabisa, lakini walimwengu wanahitajia watu kama ripota  huyo maalumu ili kuangazia ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanyika nchini humo. Amesisitiza kuwa hatua hizo bila shaka zitasaidia pakubwa katika kuiwajibisha serikali ya Kanada katika uwanja huo.

Wenyeji wa Kanada walikuwa ndio wakaazi asilia wa ardhi hiyo kabla ya kugunduliwa Amerika katika karne ya 15 Milaadia, na ambao kwa karne nyingi wamekabiliwa na matatizo mengi yaliyosababishwa na siasa za kibaguzi za serikali ya Kanada, kama tunavyoshuhudia kwamba Sheria ya Wenyeji wa Kanada ilibuniwa mwaka 1876 kwa msingi wa ubaguzi wa rangi. Katika uwanja huo, kugunduliwa makaburi ya umati nchini Kanada katika miaka ya karibuni limegeuka kuwa suala zito na muhimu linalojadiliwa na waliowengi ulimwenguni.

Ushahidi wa kihistoria na kugunduliwa makaburi ya umati katika mikoa tofauti ya Kanada unathibitisha wazi kwamba kwa miongo kadhaa, siasa kuu za serikali na Kanisa Katoliki zilikuwa ni kupora ardhi na rasilimali za wenyeji, kutenganisha watoto na familia zao pamoja na kuharibu lugha, tamaduni, mila na ustaarabu wao. Siasa hizo zilitekelezwa kwa kuwatenganisha watoto wa wakazi asilia na familia zao na kisha kuwalazimisha kuishi kwenye shule za bweni ambapo walibadilishwa fikra na kulazimishwa kuiga tamaduni za wageni waliowakoloni.

Wengi wa watoto hao walikabiliwa na unyanyasaji, ubakaji, ulawiti na utapiamlo katika shule hizo, kiasi kwamba mamia yao walikufa kwa magonjwa, utapiamlo na kupuuzwa hali zao za kiafya na kisha kuzikwa kwenye makaburi mahsusi au ya umati bila kutajwa majina wala anwani yoyote. Kugunduliwa kwa makaburi hayo ya umati katika miaka ya hivi karibuni ni ushahidi tosha wa uhalifu uliofanyika, hivyo Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Canada amekutaja kugunduliwa makaburi hayo kuwa ukumbusho wa "sura ya giza na ya aibu" ya historia ya nchi na tukio la kutisha ambapo Tume ya Kutafuta Ukweli na Maridhiano pia imeutaja ukatili huo kuwa ni mauaji ya kimbari ya kiutamaduni.

Kugunduliwa makaburi hayo ya halaiki kumeibua hisia nyingi, na licha ya jitihada za serikali ya Kanada za kujaribu kulibebesha kanisa peke yake lawama za jinai hiyo ya kutisha, lakini hatimaye kanisa na serikali ya Kanada zimelazimika kuomba msamaha pamoja, kutokana na unyama huo.

Katika safari yake ya karibuni huko Kanada Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, aliyataja mauaji ya watoto wa kiasili nchini Kanada kuwa ni "mauaji ya halaiki" na kuomba msamaha kwa wazawa asilia wa nchi hiyo kutokana na mauaji hayo yaliyofanywa katika shule za bweni za Kanisa Katoliki.

Makaburi mengine kama hayo yanaendelea kugunduliwa katika sehemu nyingine za Kanada.

"Williams Lake wa Kwanza," mmoja wa wanachama wa jamii za asili za Kanada, anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Timu moja ya utafiti imepata makaburi mengine 66 ya watu wa asili katika shule ya zamani ya makazi katika jimbo la British Columbia, hivyo idadi ya makaburi yaliyogunduliwa katika shule ya St. Joseph inafikia makaburi 159.

Watoto waliouawa katika shule za bweni za Kanisa Katoliki nchini Kanada wakumbukwa

Kwa hakika kugunduliwa makaburi hayo kunathibitisha wazi tabia ya ubaguzi na kukanyagwa hadharani nara za eti kuwepo usawa na kuheshimiwa haki za binadamu katika nchi za Magharibi, licha ya kuwepo madai yote yanayotolewa katika uwanja huo. Ukweli uliopo unaonyesha kwamba wazawa asilia, watu wa rangi na waliowachache kidini na kijamii wanakandamizwa na kuishi katika madhila makubwa katika nchi za Magharibi. Kwa kadiri kwamba kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa karibuni, wengi wa wakazi asilia wapatao milioni moja na laki mbili wa Kanada wanaishi katika hali mbaya ya kiuchumi. Hubaguliwa katika nafasi za ajira na fursa nyingine za kijamii, kadiri kwamba wengi wao wanakabiliwa na umaskini wa kupindukia, na hivyo wengi huamua kujitoa uhai au kutumbukia kwenye shimo refu la uraibu wa mihadarati.

Ivan Zinger, mkaguzi mrekebishaji wa Kanada, anasema kuhusu suala hilo: "Idadi ya watu weusi katika vituo vya kurekebisha tabia imeongezeka, na hali zao pia zimekuwa mbaya zaidi ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita. Kwa kweli, matatizo na vikwazo vya kimfumo vimekuwepo tangu zamani."

Sasa, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa ameanzisha uchunguzi katika mauaji ya watu wa asili wa Kanada, katika hali ambayo rekodi ya haki za binadamu ya nchi hiyo ni mbaya sana, na bila shaka unyanyasaji dhidi ya wenyeji asilia wa Kanada ni mojawapo ya ukiukaji huo wa haki za binadamu.


342/