Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Machi 2023

13:56:54
1350202

Makumi ya watu wauawa katika mapigano kaskazini mwa Somalia

Raia wasiopungua 210 wameuawa katika mapigano yaliyotokea huko Somaliland (eneo linalojitenga kaskazini mwa Somalia), kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya makundi yanayoiunga mkono serikali ya Mogadishu na wapiganaji wanaotaka kujitenga. Mapigano hayo yanaendelea tangu siku 24 zilizopita katika eneo hilo.

Meya wa mji wa Las Anod, Ibrahim Ali Ismail, amewaambia waandishi wa habari kuwa "raia 210 wameuawa na wengine 680 wamejeruhiwa katika mji huo unaozozaniwa na vikosi vya Somaliland na wapiganaji wa eneo linalojitawala la Puntland."

Awali Mkurugenzi wa Hospitali ya Las Anod ilisema kuwa watu 96 walikuwa wameuawa katika mapigano hayo.

Eneo la Somaliland hapo awali lilikuwa chini ya utawala wa Uingereza, kabla ya kutangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991, katika hatua ambayo haijatambuliwa na jamii ya kimataifa.

Mvutano umeibuka katika miezi ya hivi karibuni, na kusababisha mapigano kati ya vikosi vya Somaliland na vikundi vinavyoitii serikali ya Somalia, haswa katika eneo la Las Anod.

Ghasia za sasa zilizuka siku 24 zilizopita, tarehe sita Februari, saa chache baada ya viongozi wa kikabila kuchapisha taarifa ya kuahidi kuunga mkono "umoja na Jamhuri ya Shirikisho la Somalia," na kuitaka Somaliland kuondoa vikosi vyake katika eneo la Las Anod.

Nchi kadhaa za Kiarabu na Kimagharibi zimetoa taarifa ya pamoja zikitaka kusitishwa mapigano huko Las Anod, kuruhusu misaada ya kibinadamu, na kushiriki katika mazungumzo yenye kujenga na ya amani.


342/