Main Title

source : Parstoday
Jumapili

5 Machi 2023

15:54:13
1350710

US yaendelea kuiba mafuta ya Syria licha ya kukumbwa na zilzala

Marekani kwa kushirikiana na mamluki wa Kikurdi imeendelea kuiba mafuta ya Syria, wakati huu ambapo nchi hiyo ya Kiarabu inajaribu kujinasua kutoka kwenye misukosuko na changamoto zinazotokana na matetemeko ya ardhi yaliyoua maelfu ya watu nchini humo.

Vyanzo vya habari vimeviambia vyombo vya habari vya Syria kuwa, msafara wa malori 23 yaliyokuwa yamebeba mafuta ya wizi ya Syria ulionekana ukitokea eneo lenye visima vya mafuta la al-Jazeera eneo la al-Yarubiya, na kuingia Iraq kupitia mpaka haramu wa al-Mahmudiya. 

Habari zaidi zinasema kuwa, msafara mwingine wa malori na vifaru 34 vya Marekani ulionekana ukiingiza mafuta ya wizi nchini Iraq kupitia kivuko haramu cha al-Walid.

Marekani inaendelea kuiba mafuta na rasimali za Syria katika hali ambayo, hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitaja matetemeko ya ardhi yaliyoitikisa nchi hiyo na jirani yake Uturuki kuwa ni janga la baya zaidi la kimaumbile katika karne moja ya karibuni.

Nalo  Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limesema linahitaji dola milioni 172.7 ili kutoa msaada wa haraka wa kuokoa maisha kwa watu milioni 5.4, wakiwemo watoto milioni 2.6, walioathiriwa na tetemeko la ardhi huko Syria.

Mbali na wizi wa mafuta, Marekani na waitifaki wake wamekuwa wakikwamisha shughuli za kufikisha misaada ya dharura na kibinadamu kwa waathirika wa zilzala nchini Syria.

Wasyria zaidi ya 6,700 wamepoteza maisha huku wengine karibu 15,000 wakijeruhiwa kwenye mitetemeko hiyo ya ardhi iliyozikumba Syria na Uturuki mwezi uliopita.

342/