Main Title

source : Parstoday
Jumatano

8 Machi 2023

07:36:23
1351159

Mchango wa NATO katika kuimarika magaidi barani Afrika

Uwepo wa makundi ya kigaidi amilifu katika maeneo mbalibali barani Afrika hususan katika eneo la Sahel Afrika umekuwa tatizo na kikwazo cha kurejesha amani katika mataifa ya aeneo hilo.

Harakati za makundi ya kigaidi katika maeneo hayo zimekuwa zikitumiwa kama kisingizio na madola ya kigeni cha kuingilia masuala ya ndani ya mataifa ya Kiafrika.

Abdolaye Diop, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Mali amesema kuwa, uingiliaji wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) umepelekea kuimarika na kupata nguvu magaidi katika nchi hiyo na nchi zote za eneo la Sahel Afrika kwa ujumla.

Pamoja na kuwa nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto nyingi katika nyuga mbalimbali kama za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiusalama, lakini uwepo wa makundi ya kigaidi katika bara hilo na wasiwasi wa kuongezeka harakati zao katika mataifa tofauti, filihali hiyo imegeuka na kuwa moja ya daghadagha na wasiwasi mkubwa wa nchi za bara hilo.

Kuhusiana na hilo, uwepo wa kundi la kigaidi la Boko Haram magharibi mwa Afrika hususan nchini Nigeria na mataifa yanayopakana nayo, na vilevile harakati za kundi la wanamgambo wa al-Shabab mashariki mwa Afrika hususan Somalia na nchi zinazopakana nayo na kadhalika kuweko makundi ya kigaidi kama Daesh katika eneo la Sahel Afrika ni mambo ambayo yamehatarisha usalama wa bara hilo na kutishia amani yake siku baada ya siku.Hali hiyo inashuhudiwa katika hali ambayo, katika miaka ya hivi karibuni madola mbalimbali ya Kimagharibi yametuma vikosi vyake katika nchi tofauti za Kiafrika kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Ufaransa ni mtoa madai mkuu kuhusiana na jambo hili. Mamia ya askari wa Ufaransa walikuweko katika mataifa ya Sahel Afrika hususan nchini Mali na Burkina Faso. Uwepo wa askari hao wa kigeni haujawa na faida yoyote ile katika kudhamini amani na usalama na badala yake harakati za kigaidi zimeshuhudiwa zikichukua wigo mpana zaidi siku baada ya siku. Utendaji mbovu wa vikosi vya Ufaransa uliifanya serikali ya Burkina Faso hivi karibuni ichukue uamuzi wa kukomesha ushirikiano wake wa kijeshi na Paris na hivyo kuvitimua vikosi vya taifa hilo katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiafrika. Ukweli wa mambo ni kuwa, vita dhidi ya ugaidi ni kisingizio kinachotumiwa na madola yaa magharibi kwa ajili ya kuhalalisha uwepo wake wa kijeshi katika bara tajiri la Afrika. Hii ni katika hali ambayo, akthari ya matatizo ya sasa ya nchi za Kiafrika chimbuko lake ni utendaji mbaya na uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya mataifa hayo. Kwa mfano uingiliaji wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO huko Libya umeifanya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kugeuka na kuwa kituo kikuu cha kujiimarisha makundi ya kigaidi barani Afrikka. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa Hivi karibuni Emmanuel Macron wa Ufaransa aliashiria uingiliaji wa kijeshi wa Ufaransa nchini Libya mwaka 2011 na kuutaja kuwa lilikuwa kosa. Macron aliongeza kusema kama ninavyomnukuu: Ufaransa iliingilia masuala ya ndani ya Libya bila ya kuzingatia maoni na mitazamo ya wananchi nchi hiyo ambapo uingiliaji huo hatimaye ulihitimisha utawala wa kanali Muammar Gaddafi, hivyo sisi hatukuheshimu kabisa mamlaka ya kujitawala taifa hilo. Kuhusiana na hilo, hivi karibuni kulitolewa ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyokuwa ikionesha kwamba, katika miaka ya hivi karibuni bara la Afrika limepata pigo kubwa sana kutokana na kuenea ushawishi na harakati za makundi ya kigaidi kama Daesh na al-Qaeda na makundi ya wanamgambo yaliyotangaza utiifu kwa makundi hayo. Takwimu zinaonyesha kuwa, kuanzia Januari mpaka Juni mwaka 2022, kundi la Daesh magharibi mwa Afrika lilitekeleza hujuma na mashambulio 305 na kuongezea idadi ya wahanga wa mashambulio ya kigaidi katika mataifa mbalimbali barani Afrika. Abdolaye Diop, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Mali anasema: Ukosefu wa usalama unaosababishwa na mashambulio ya kigaidi kwa sasa hauishii tu katika maeneo ya kaskazini mwa Mali, bali takribani maeneo yote ya nchi hiyo yanajumuishwa na hali hiyo, na si hivyo tu bali magaidi hao wamevuka mpaka na kuingia katika mataifa jirani na kwenda mpaka katika Ghuba ya Guinea. Alaa kulli haal, licha ya kuwa umasikini, kutokuweko vyanzo vya kutosha vya fedha na himaya na uungaji mkono wa siri na usio wa moja kwa moja wa madola ya magharibi kwa baadhi ya makundi ya kigaidi ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayolikabili bara la Afrika, lakini inaonekana kuwa, nchi za Kiafrika zimo mbioni kuongeza ushirikiano wao wa kieneo na hivyo kuendesha vita vya kistratejia na vilivyo na uratibu zaidi dhidi ya ugaidi.