Main Title

source : Parstoday
Jumapili

19 Machi 2023

19:47:49
1353066

Undumakuwili wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuhusu jinai za kivita

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, ambayo inajiona kuwa mahakama ya kwanza ya kudumu ya kimataifa inayoshughulikia uhalifu wa mauaji ya halaiki, jinai dhidi ya binadamu, jinai za kivita na uchokozi, Ijumaa iliyopita ilitoa waranti wa kimataifa wa kukamatwa Rais Vladmir Putin wa Russia.

Mahakama hiyo inadai kuwa Putin 'amehusika na uhalifu wa kivita' ikiwa ni pamoja na 'kuhamishwa watoto kinyume cha sheria kutoka maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Ukraine hadi Russia'. Mahakama hiyo pia imetoa waranti wa kukamatwa Maria Lvova Belova, kamishna wa ofisi ya Rais wa Russia anayeshughulikia masuala ya haki za watoto kwa madai kwamba pia alihusika katika uhalifu huo wa kivita. Moscow imepinga vikali tuhuma hizo na kuzitaja kuwa za 'kidhalimu'.

Suala la kushangaza na kuchekesha ni kwamba Marekani ambayo imehusika na uvamizi mkubwa wa kijeshi dhidi ya nchi nyingine huru hususan Afghanistan na Iraq na kufanya huko jinai za kila aina za kivita, imeunga mkono agizo la Putin kukamatwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Kuhusiana na hilo, Rais Joe Biden wa Marekani amesema kuwa Rais Vladimir Putin ametenda jinai za kivita huko Ukraine hivyo uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai wa kumkamata ni halali. Marekani inadai kuwa imethibitisha kufuatia uchunguzi wake huru kwamba vikosi vya Russia vimefanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

Akitoa radiamali yake kuhusiana na waranti wa kukamatwa Putin, Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema uamuzi huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai hauna maana wala taathira yoyote ya kisheria kwa nchi hiyo. Amesema Russia si mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC hivyo haiwajibishwi kivyo vyote vile na mkataba huo.

Suala muhimu kuhusu hukumu za Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ni namna inavyotumia vipimo vya ubaguzi na undumakuwili wa wazi katika kushughulikia mauala yanayohusiana na jinai za kivita. Ingawa hakuna taasisi yoyote ya kimataifa wala kundi la uchunguzi wa kimataifa lililotoa ripoti kuhusu kuhamishwa kwa nguvu watoto wa Ukraine na kupelekwa Russia, lakini Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahajama hiyo amedai kuwa suala hilo liko wazi kadiri kwamba hakuna haja ya mtu kuwa mwanasheria ili kuthibitisha kuwa limetokea! Ni wazi kuwa mahakama hiyo imeharakisha hukumu isiyo ya kawaida ya kukamatwa Rais Putin wa Russia kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita bila kuzingatia wala kufuata hatua zinazotakikana kisheria.

Hii ni pamoja na kuwa licha ya kuthibitishwa wazi jinai za kivita zilizotendwa na Marekani huko Afghanista na Iraq lakini mahakama hiyo ilitangaza hadharani kuwa haitashughulikia kesi hizo. Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, Desemba 2021, ikiwa ni katika juhudi za kuhalalisha hatua yake ya kutofuatilia jinai za kivita za Marekani nchini Afghanistan, alisema: 'Nimefanya uamuzi huu kwa kuzingatia ushahidi kwamba jinai kubwa zaidi kwa mtazamo wa makali, ukubwa na kiwango hazikufanywa na jeshi la Marekani.' Kabla ya hapo Karim Khan alikuwa amesema kwamba vitendo vya Taliban na Daesh kuhusu jinai za kivita na uhalifu wa haki za binadamu nchini Afghanistan ulikuwa unafuatiliwa kwa karibu na mahakama hiyo iliyo na makao makuu yake huko The Hague Uholanzi. Mahakama ya ICC ilianzisha uchunguzi wa awali kuhusu uhalifu wa kivita nchini Afghanistan mwaka 2006, na mwaka 2017, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama hiyo, Fatou Bensouda, aliwataka majaji wa mahakama hiyo kuidhinisha uchunguzi kamili katika uwanja huo, ikiwa ni pamoja na utendaji wa askari wa Marekani na NATO nchini Afghanistan.

Hata hivyo, vikwazo vya Marekani dhidi yake na maafisa wengine wa mahakama hiyo wakati wa urais wa Donald Trump vilisababisha mahakama hiyo kutafakari upya uamuzi wake wa awali katika uwanja huo. Mashirika ya haki za binadamu yamekosoa mara kwa mara ukweli kwamba jinai za kivita za Marekani zinafumbiwa macho na mahakama hiyo ya jinai. Miongoni mwa mashirika mengine, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilikosoa vikali uamuzi wa mahakama ya The Hague wa kuiondoa Marekani katika uchunguzi wa jinai za kivita kutokana na tishio la Ikulu ya Marekani la kuiwekea vikwazo, na kutaka uchunguzi wa pande zote ufanyike dhidi ya nchi hiyo, vikiwemo vitendo vya jeshi lake dhidi ya watu ya Afghanistan.

Suala jengine ni kwamba ikiwa rais wa nchi atafunguliwa mashtaka ya kufanya uhalifu wa kivita, basi rais wa kwanza anayetakiwa kufikishwa kizimbani kutokana na uhalifu huo ni George W. Bush, rais wa zamani wa Marekani ambaye alitoa amri ya kuvamiwa kijeshi Afghanistan na Iraq ambapo maelfu ya watu wasio na hatia katika nchi hizo mbili waliuawa kinyama. Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Magharibi, akiwemo George W. Bush na Tony Blair, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, ambao waliamuru kuvamiwa Iraq mwaka 2003, hawajafunguliwa mashtaka  ya aina yoyote ile na mahakama ya ICC.

342/