Main Title

source : Parstoday
Jumanne

21 Machi 2023

09:23:24
1353251

Kutimia miaka 20 ya shambulio la Marekani dhidi ya Iraqi: Nembo ya sera za vita na maamuzi ya upande mmoja

Miaka 20 iliyopita, Machi 20, 2003, George W. Bush, Rais wa Marekani, aliamuru mashambulizi dhidi ya Iraq bila idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwa hatua ya upande mmoja na kinyume cha sheria kwa ushirikiano wa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair. Majeshi ya Marekani na Uingereza yalianzisha vita vikubwa dhidi ya Iraq na kupelekea kuanguka utawala wa Baath ulioongozwa na dikteta Saddam.

Kisingizio kikuu kilichotumiwa na Bush na Blair kuanzisha vita hivyo kilikuwa ni kuharibu vituo vya kutengeneza silaha za maangamizi ya umati (WMDs). Hata hivyo, licha ya madai ya mashirika ya kijasusi ya Marekani na Uingereza, hakuna silaha za maangamizi makubwa zilizopatikana nchini Iraq baada ya kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya nchi hizo mbili. Matokeo ya awali kabisa ya vita hivyo yalikuwa ni kuuawa makumi ya maelfu ya Wairaqi wasio na hatia.

Nukta muhimu ni kwamba hivi sasa, katika mwaka wa 20 tangu vianzishwe vita dhidi ya Iraq, matokeo ya uchunguzi wa maoni miongoni mwa Wamarekani yanaonesha kuwa wengi wao wanaamini kuwa vita hivyo vilipelekea kupungua usalama wa kitaifa wa Marekani.

Wakati theluthi mbili ya Wamarekani waliidhinisha hatua za kijeshi dhidi ya Iraq mwaka 2003, asilimia 61 sasa wanaamini kuwa uamuzi huo haukuwa sahihi.

Kuhusiana na hilo, na sambamba na kumbukumbu ya kutimia miaka 20 ya uvamizi wa Marekani nchini Iraq, maelfu ya watu wanaopinga vita na uchochezi wa kijeshi wa serikali ya Marekani walifanya maandamano Jumamosi mjini Washington. Waandalizi wa maandamano hayo wameeleza kuwa madhumuni ya mkusanyiko na maandamano hayo ni kuelimisha watu kuhusu madhara ya vita na pia kuwafahamisha kuhusu hasara za kibinadamu zinazotokana na sera za kivita za Marekani duniani. Nchini Uingereza pia wananchi waliowengi nao pia wamebainisha upinzani wao mkubwa kwa sera za kivita za serikali ya nchi hiyo.

Don Jarvis, ambaye alihudumu katika jeshi la Uingereza nchini Iraq na sasa ni mwakilishi wa Chama cha Labour, anasema: uharibifu uliosababishwa katika vita dhidi ya Iraq umevuruga imani ya umma.

Uvamizi wa kijeshi wa Iraq ulisababisha vifo vya maelfu kadhaa ya wanajeshi wa Kimarekani pamoja na hasara kubwa kwa watu wa Iraqi mbali na kuathiri vibaya uchumi wa Marekani na itibari ya kimataifa ya nchi hiyo.

Uchunguzi umebaini kuwa, uvamizi wa Marekani dhidi ya Iraq kwa kushirikiana na Uingereza na kisha hatua ya nchi hizo mbili ya kuendelea kuikalia kwa mabavu Iraq ulisababisha vifo vya raia wasiopungua 210,000. Baada ya vita hivyo, Iraq ilikumbwa na ukosefu wa utulivu na usalama kwa muda mrefu na ikawa jukwaa la magaidi wakufurishaji  ambapo  maeneo mengi ya kaskazini mwa nchi hiyo yalidhibitiwa kwa miaka kadhaa na kundi la kigaidi la ISIS baada ya kuondoka wanajeshi vamizi wa Marekani mnamo 2011.

Miaka kadhaa baada ya serikali ya Iraq kuamuru kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani, bado kuna wanajeshi wa Marekani wapatao 2,500 ambao wamesalia nchini humo kwa visingizo mbali mbali. Kwa mujibu wa takwimu ya Pentagon, jumla ya majeruhi wa kijeshi wa Marekani katika vita vyote vya Iraq ilifikia 4,487.

Wakati wa uvamizi wa Iraq, Bush alidai kuwa shambulio hilo lilianzishwa ili kuipokonya Iraq silaha za maangamizi ya umati na kuwakomboa watu wake, ili ulimwengu uondokane na hatari kubwa. Baada ya kuangushwa utawala wa Baath wa Saddam, Marekani ilitangaza kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wa vita vya Iraq.

Lakini ukweli ni kwamba vita vya Marekani dhidi ya Iraq kivitendo viliendelea kwa miaka kadhaa, ambapo makumi ya  maelfu ya watu waliuawa na kujeruhiwa. Mbali na gharama za kibinadamu za vita vya Iraq, vita hivyo pia viliacha gharama kubwa ya kifedha, kama ilivyofichuliwa na ripoti nyingi zilizochapishwa na taasisi za utafiti nchini Marekani.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Kituo cha Utafiti cha Kennedy katika Chuo Kikuu cha Harvard ambacho kilitangaza katika ripoti yake ya 2013 kwamba vita vya Iraq na Afghanistan ni vita vilivyokuwa na gharama kubwa zaidi katika historia ya Marekani na kwa ujumla viligharimu kati ya dola trilioni nne hadi sita, ambayo ni sawa na dola 75,000 kwa kila familia ya Marekani. Hali mbaya ya hivi sasa ya kifedha ya serikali ya Marekani, hasa katika suala la nakisi ya bajeti na deni la taifa, inasababishwa kwa kiasi kikubwa na vitendo vya kivita vya tawala za Bush na Obama huko Iraq na Afghanistan.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Michael Hirsh aliandika katika Jarida la Foreign Policy kwamba: Shambulio dhidi ya Iraq lilikuwa mojawapo ya makosa muhimu ya kimkakati katika historia ya Marekani. Maafa ya kujitakia huko Iraq yalifichua udhaifu wa kijeshi wa Marekani na kufundisha ulimwengu mzima jinsi ya kushinda na kupigana na kile ambacho hapo awali kilichukuliwa kuwa nguvu kuu isiyoweza kupingwa ya Marekani.