Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

30 Machi 2023

13:50:20
1355020

Ripoti ya China kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu Marekani

China imetoa ripoti yake kuhusu hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Marekani katika mwaka uliopita wa 2022.

Katika ripoti yake hiyo, Beijing imeashiria kuporomoka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hali ya haki za binadamu nchini Marekani na kuikosoa Washington kwa kupuuza haki za kimsingi na uhuru wa watu wa Marekani.

Mifano ya masuala kama ubaguzi wa rangi, ukatili wa utumiaji silaha, ukatili na ukandamizaji unaofanywa na Polisi na mgawanyo usio wa haki wa utajiri wa taifa nchini Marekani, imeashiriwa kwa wingi katika ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne na Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali ya China, ikiwa na anwani "Ripoti ya Ukiukwaji wa Haki za Binadamu nchini Marekani mwaka 2022".

Katika sehemu nyingine ya ripoti hiyo ya China kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa nchini Marekani imeelezwa kwamba, demokrasia ya mtindo wa Marekani imepoteza nafasi yake mbele ya umma na baadhi ya misaada ya kifedha inatolewa kwa lengo la kubadilisha kwa siri matokeo ya uchaguzi nchini humo. Ripoti hiyo imeongezea kwa kusema: watu nchini Marekani ndio walengwa wa vitisho vya vyombo vya utekelezaji sheria, wakati Marekani yenyewe inajionyesha kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu.

Serikali ya China huchapisha ripoti ya kila mwaka kuhusu hali mbaya ya haki za binadamu nchini Marekani, ambayo inalenga kuangazia uongo wa madai ya watawala wa Washington kuwa eti ni watetezi wa haki za binadamu. 

Ripoti ya kila mwaka ya China kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Marekani inajaribu kueleza hali halisi ya utendaji wa watawala wa Washington katika kadhia ya haki za binadamu hasa utendaji mbovu wa utawala huo dhidi ya Wamarekani wasio wazungu. Ripoti hiyo pia inawezesha umma wa dunia hufahamu hali mbaya ya haki za binadamu iliyoko nchini Marekani.

Stephen Landman, mtafiti katika Kituo cha Marekani cha Utafiti wa Utandawazi, anasema,

Marekani ni demokrasia ya maneno tu, lakini kiutendaji, ikiwa na maelfu ya wafungwa, ndiyo yenye idadi kubwa ya magereza na ndiyo mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu duniani. Baada ya Septemba 11, 2001, George Bush, akiwa afisa mkuu mtendaji alitangaza sera ya utesaji kuwa halali, na hii ni sera ambayo ilikiuka haki za watu wengi wakiwemo Waislamu.

Licha ya madai yake ya kutetea haki za binadamu, serikali ya Marekani ina rekodi mbaya sana katika kuzingatia viwango vya haki za binadamu, na inakiuka waziwazi haki  za binadamu nje ya mipaka yake, moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Kuchochea na kuendesha vita dhidi ya nchi nyingine, hasa Iraq na Afghanistan, ni moja ya ukiukwaji wa moja kwa moja wa haki za binadamu uliofanywa na Marekani katika uga wa kimataifa.

Utekelezaji wa vikwazo vya upande mmoja, hasa vikwazo vya dawa, dhidi ya nchi huru na  zinazopinga sera za kivita na kibeberu za Marekani ni mojawapo ya ukiukaji wa moja kwa moja wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya China,  Marekani imekiuka haki za binadamu kimataifa kwa kuweka vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi zaidi ya 20 duniani, ikiwemo Cuba tangu mwaka 1962, Iran tangu mwaka 1979, Syria tangu mwaka 2011 na Afghanistan katika miaka ya hivi karibuni.

Upana na undani wa sera za Marekani dhidi ya haki za binadamu ndani na nje ya nchi hiyo umeifanya Marekani ijulikane kuwa mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani.

Serikali ya Marekani imeligeuza suala la haki za binadamu kuwa chombo cha kutoa mashinikizo ya kisiasa na kuanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya nchi zinazopinga ubeberu wa utawala wa Ikulu ya White House.

Nukta chanya ni kuwa Marekani imepoteza itibari yake kutokana na jinai zake na hivi sasa mataifa mengi duniani hayaamini tena madai bandia ya Marekani kuwa eti ni mtetezi wa haki za binadamu.


342/