Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

30 Machi 2023

13:51:14
1355022

China yaonya, tutatoa jibu Rais wa Taiwan akikutana na Spika wa US

China imeionya vikali Washington na kusisitiza kuwa itachukua 'hatua ya kujibu mapigo' iwapo Rais wa Taiwan, Tsai Ing-wen atakutana na Spika wa Kongresi ya Marekani, Kevin McCarthy katika safari yake inayotazamiwa kufanyika karibuni.

Zhu Fenglian, Msemaji wa Baraza la Kusimamia Masuala ya Taiwan lenye makao yake Beijing amesisitiza kwamba, mkutano tarajiwa wa Rais wa Taiwan na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani mjini Washington mwezi ujao utakuwa na matokeo mabaya.

Amebainisha kuwa, "Iwapo (Rais wa Taiwan) atakutana na Spika wa Marekani, McCarthy, huo utakuwa ni uchokozi mwingine ambao utakiuka vibaya kanuni ya 'China Moja' mbali na kukanyaga mamlaka ya kujitawala China, na pia kusambaratisha amani na uthabiti katika Lango Bahari la Taiwan." 

Fenglian amesema mkutano huo hautakuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha mivutano na mikwaruzano baina ya Marekani na China, na kwamba Beijing haitafumbia macho uchokozi huo. Hata hivyo hajaeleza aina ya jibu litakalotolewa na China mkabala wa Marekani.

Itakumbukwa kuwa, Agosti mwaka jana, China ilifyatua makombora kadhaa ya balestiki kuelekea maji yanayoizunguka Taiwan katika mazoezi makubwa ya kijeshi kuwahi kushuhudiwa, likiwa ni jibu kwa ziara iliyofanywa na Spika wa wakati huo wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi katika kisiwa hicho.

Serikali ya Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China na haijafuta uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi ili kushika hatamu za udhibiti wa kisiwa hicho.

China imeshaionya Marekani mara kadhaa kwamba haitakuwa tayari kufanya maridhiano yoyote juu ya suala la Taiwan na itatoa jibu kali kwa chokochoko zozote zitakazofanywa juu ya suala hilo.

342/