Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

30 Machi 2023

13:51:50
1355023

Nchi za Asia Kusini zapania kuachana na matumizi ya dola, yuro

Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) inatazamiwa kujadili mpango wa kuachana na matumizi ya sarafu ya dola ya Marekani na yuro ya Ulaya katika miamala yao ya kibiashara.

Kwa mujibu wa jarida la habari la Tempo, kadhia hiyo ya kuziweka pembeni sarafu hizo za Magharibi itajadiliwa kwenye mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya kieneo unaofanyika huko Indonesia.

Iwapo azma hiyo itapasishwa kwenye mkutano wa jumuiya ya ASEAN, basi nchi wanachama wake ambazo ni Brunei, Cambodia, Indonesia, Laos, Malaysia, Myanmar, Ufilipino, Singapore, Thailand, na Vietnam, zitaachana na matumizi ya dola na yuro, na badala yake zitumie sarafu za ndani ya nchi hizo.

Duru za habari zinaarifu kuwa, mkutano huo utajadili mpango huo chini ya anuani ya 'kupunguza utegemezi wa sarafu kubwa za kigeni, na kufanya miamala kwa kutumia sarafu za ndani.'

Tayari nchi kadhaa wanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda kama Indonesia, Malaysia, Singapore na Thailand zimeanza kufanya mabadilishano ya kibiashara kwa kutumia sarafu za kitaifa za nchi hizo.

Katika miaka ya hivi karibuni, Russia na baadhi ya washirika wake wa kibiashara, ikiwa ni pamoja na Iran, India na China, zimekuwa zikiimarisha matumizi ya sarafu zao za kitaifa katika biashara ili kujiondoa katika ubeberu wa dola ya Marekani na yuro ya bara Ulaya.

Nchi kadhaa za Afrika pia kama Sudan, Ghana na Zimbabwe zimeandaa sera mpya ya kununua bidhaa kama vile za mafuta kwa kutumia dhahabu badala ya sarafu ya dola ya Marekani. 

342/