Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

1 Aprili 2023

13:16:31
1355331

Seneti ya Marekani yafuta kibali cha Pentagon kuhusu oparesheni za kijeshi Iraq

Seneti ya Marekani Jumatano wiki hii ilihitimisha kibali ilichokuwa imekitoa kwa Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) mwaka 1999 na 2002 kwa ajili ya vita huko Iraq na imepasisha uamuzi wa kufutwa kibali cha Pentagon kwa ajili ya kutekeleza oparesheni za kijeshi huko Iraq bila ya kuhitaji idhini ya Kongresi.

Wajumbe 54 wa Bunge la Seneti la Marekani walipasisha kura ya kufuta  sheria hiyo mkabala wa wajumbe wengine 27 waliopinga. Sheria hiyo ilikuwa ikiiruhusu Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kufanya oparesheni za kijeshi ndani ya ardhi ya Iraq kwa amri ya Rais tu na bila ya kuhitaji kibali cha Kongresi.   

Mark Warner mjumbe wa chama cha Democrat katika Seneti ya Marekani anayeliwakilisha jimbo la Virgina amezungumzia kadhia hiii akisema: Imechukua muda mrefu hadi Kongresi kupata mamlaka yake ya kutangaza vita; na ninajivunia kupasisha sheria ya kufutwa kibali cha kutumiwa nguvu za kijeshi huko Iraq." 

Sheria hiyo imetumwa kwa Bunge la Wawakilishi kwa ajili ya kupasishwa; na hii inahesabiwa kuwa hatua kubwa na muhimu katika kuirejeshea Kongresi haki ya kutoa maamuzi juu ya wakati gani Marekani inaweza kutuma wanajeshi vitani. Hapo awali, wakati ilitarajiwa kuwa Baraza la Seneti la Marekani lingepiga kura ya kuondoa sehemu ya mamlaka katika sheria inayoidhinisha hatua za kijeshi nchini Iraq, iliyotumiwa na Marekani kuivamia Iraq na kuuondoa madarakani utawala wa Saddam, baadhi ya Warepublican walieleza wasiwasi wao kuhusu suala hili. Sheria hiyo bado ilikuwa bado inatumiwa na Pentagon kuhalalisha oparesheni zake za kijeshi nchini Iraq licha ya kupita miaka 20 tokea Marekani iivamie kijeshi na kuikalia kwa mabavu Iraq. Hatua ya kwanza ya kufutilia mbali sheria hiyo ilichukuliwa na Seneti ya Marekani wiki mbili zilizopita, na baada ya vikao kadhaa vya majadiliano, Seneti ilipanga kupiga kura Jumatano iliyopita ili kufutilia mbali kibali hicho.  

Wakati huo huo Chuck Schumer kiongozi wa Wademocrat ndani ya Seneti amekaribisha hatua hiyo aliyoitaja kuwa ya dharura kwa ajili ya kuweka kando masalia ya vita huko Iraq na akasema kwamba: "Wananchi wa Marekani wamechoshwa na vita visivyokwisha katika eneo la Mashariki ya Kati." 

Serikali ya Biden kwa upande wake inasema kuwa inaunga mkono kufutwa sheria hiyo ambayo ilipasishwa na Rais wa zamani wa Marekani, George W.Bush, na kwamba itahakikisha kuwa suala hilo halitakuwa na athari zozote kwa oparesheni za sasa. Hata hivyo gazeti la Washington Post limeandika katika ripoti yake kuwamba, Warepublican wameeleza wasiwasi wao katika uwanja huo kwa visingizio mbalimbali kama eti vitisho kutoka Iran. Hii ni katika hali ambayo Iran imekuwa na nafasi muhimu katika kuhakikisha kuwa Iraq inakuwa na amani na utulivu na imetoa mchango mkubwa katika kupambana na kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh huko Iraq. Ni wazi kuwa kuwepo vikosi vya majeshi vamizi ya Marekani huko Iraq kunachochea moto wa vita na hali ya mchafukoge nchini humo.  

Rais wa wakati huo wa Marekani, George W. Bush tarehe 20  Machi 2003 alichukua uamuzi wa upande mmoja na kinyume cha sheria, akishirikiana na Tony Blair, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza na kuamuru kushambuliwa Iraq. Wanajeshi wa Marekani na Uingereza waliendesha vita vikubwa nchini Iraq ambavyo vilipelekea kuenguliwa madarakani utawala wa Baath na kumuondoa madarakani Saddam Hussein. Bush alidai wakati huo alipoivamia Iraq kwamba, Marekani imeishambulia Iraq ili kuiponya nchi hiyo silaha za maangamizi ya halaiki na kuwakomboa watu wa nchi hiyo ili kuiepusha dunia na hatari. Bush alitangaza kufikia ukomo vita vya Iraq baada ya Marekani kupata ushindi wa awali nchini humo na kuuangushwa utawala wa Baath.

Ukweli wa mambo ni kuwa vita vya Marekani dhidi ya Iraq, ambavyo viliendelea kwa kipindi cha miaka kadhaa, viligeuka na kuwa vita vya muda mrefu ambapo maelfu ya Wairaqi waliuawa na makumi ya maelfu ya wengine walijeruhiwa. Kukaliwa kwa mabavu Iraq mbali na kusababisha vifo vingi vya wananchi wa Iraq kulipelekea pia kuuliwa maelfu  kadhaa ya wanajeshi wa Marekani na kusababisha gharama na hasara kubwa kwa uchumi na hadhi ya Marekani kimataifa. 

Uvamizi wa Marekani na Uingereza huko Iraq baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo ulipelekea kuuliwa raia wasiopungua 210,000. Baada ya vita hivyo, Iraq ilitumbukia katika hali ya mchafukoge kwa muda mrefu na kuwa kitovu cha magaidi wa kitakfiri. Aghalabu ya maeneo ya kaskazini mwa Iraq yalitumbukia mikononi mwa kundi la kigaidi la Daesh baada ya vikosi vamizi vya Marekani kuondoa baadhi ya wanajeshi wake huko Iraq mwaka 2011. Wanajeshi karibu 2,500 wa Marekani bado wapo Iraq licha ya kupita miaka kadhaa tokea serikali ya Iraq iagize kuondoka nchini humo vikosi vamizi vya Marekani.

Wakati huo huo takwimu za Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) zinaonyesha kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo 4,487 wamepoteza maisha katika vita vya Iraq. Ni dhahir shahir kuwa hali mbaya ya kifedha inayoikabil serikali ya Marekani hasa kwa upande wa nakisi ya bajeti na madeni iliyonayo imesababishwa kwa kiasi kikubwa na hatua za kupenda vita na mabavu za serikali za Bush na Obama huko Iraq na Afghanistan.    


342/