Main Title

source : Parstoday
Jumapili

2 Aprili 2023

13:55:40
1355572

Russia yapinga vitendo vya uchochezi vya Marekani nchini Syria

Kamanda wa ngazi za juu nchini Russia alitangaza siku ya Ijumaa kuwa Moscow iimelalmikia "vitendo vya uchochezi" vya vikosi vamizi vya Marekani nchini Syria.

Admeri Oleg Gurinov, Mkuu wa Kituo cha Russia cha Maridhiano ya Pande Zinazohasimiana nchini Syria, ameandika kwamba Russia imesajili vitendo vya uchochezi vya Wamarekani katika mkoa wa Hasaka kaskazini mwa Syria. Majeshi ya Marekani yameonekana mara mbili nje ya maeneo yaliyokubaliwa. Russia imewasilisha malalmiko yake kwa muungano wa kijeshi unaongozwa na Marekani kuhusu ukiukaji huo.

Afisa huyo mkuu wa kijeshi wa Russia ameonya kwamba ukiukaji wa makubaliano ya kijeshi kati ya Russia na muungano unaoongozwa na Marekani utahatarisha mlingano dhaifu wa mamlaka uliopo katika eneo hilo na utakuwa na athari mbaya. Zaidi ya wiki moja iliyopita vyombo vya habari viliripoti shambulio la mabomu katika maeneo ya Mkoa wa Deir Ezzor mashariki mwa Syria. Saa chache baadaye, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilithibitisha kutokea shambulio la anga kwenye mji wa Deir Ezzor mashariki mwa Syria. Baada ya hayo, Rais Joe Biden wa Marekani katika barua yake kwa Bunge la Congress la nchi hiyo alidai kuwa, mashambulizi dhidi ya maeneo ya harakati za muqawama mashariki mwa Syria yamefanywa kwa mujibu wa haki ya kujilinda na kutishia kuwa, ikibidi hatua zaidi zitachukuliwa.

Marekani inasisitiza juu ya kuendelea kuwepo kijeshi kinyume cha sheria nchini Syria na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Kuhusiana na hilo, baada ya ufyatulianaji risasi kati ya wanajeshi wa Marekani wanaoikalia kwa mabavu Syria na makundi ya muqawama mashariki mwa nchi hiyo, jeshi la Marekani liliongeza muda wa kuwepo meli zake katika maji ya karibu na nchi hiyo. Siku ya Ijumaa iliyopita pia maafisa wa kijeshi wa Marekani walitangaza kuongeza muda wa uwepo wa manoari ya kivita ya "George W. Bush" katika pwani ya karibu na Syria ili iwe rahisi kutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Syria. Uamuzi huu unamaanisha kuwa msafara wa manoari za kivita unaaongozwa na manoari ya "George W. Bush," wenye zaidi ya askari wake 5,000 wa Marekani, ambao sasa wako katika maji ya Ugiriki utabakia karibu na Syria kwa muda mrefu zaidi.

Katika miaka ya hivi karibuni, majeshi ya Marekani yamekuwepo nchini Syria katika fremu ya eti muungano wa kimataifa  dhidi ya ISIS au Daesh. Hivyo Marekani imekalia kwa mabavu ardhi ya Syria kwa kisingizio cha kupambana na kundi hilo la kigaidi, lakini kivitendo, hawafanyi lolote zaidi ya kuwaua raia na kupora utajiri wa Syria hasa mafuta ghafi ya petroli.

Marekani imekuwa ikifuatilia malengo maalumu katika uwepo wake wa kijeshi nchini Syria katika kipindi cha muongo moja uliopita.

Wakati wa uongozi wa Barack Obama tangu mwaka 2011, Marekani iliunga mkono na kuyafadhili makundi ya kigaidi nchini Syria kwa lengo la kuipindua serikali halali ya Bashar al-Assad na kudhoofisha mhimili wa muqawama au harakati za ukombozi wa Palestina..

Mwaka 2014, Marekani ilianza oparesheni ya anga na nchi kavu ya kutuma askari wake vamizi nchini Syria. Baada ya Donald Trump kuingia madarakani, alidumisha uwepo haramu wa kijeshi wa Marekani nchini Syria kwa kisingizio cha kupambana na ISIS, na hata alitwaa kwa mabavu baadhi ya maeneo ya ardhi ya Syria na kupora mafuta ya nchi hiyo. Majeshi ya Marekani yamekuwepo katika maeneo ya mashariki mwa Syria, ambayo ni maeneo yenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi. Wamarekani wamekuwa wakipora mafuta ya Syria na kuyaondoa  nchini humo  kupitia ardhi ya Uturuki.

Utawala wa Biden umeendeleza mashambulizi ya anga katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita, na kupuuza sheria za kimataifa kuhusu mamlaka ya kujitawala Syria. Uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Syria unaendelea bila idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Biden amefuata sera hiyo hiyo ya kidhalimu ya Trump kulenga mhimili wa muqawama nchini Syria, na mara kwa mara, hufanya mashambulizi ya anga na makombora kwenye ngome za vikosi vya muqawama.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov anasema: Marekani inajaribu kuiweka Syria katika hali ya mgogoro na hivyo imeanzisha tena taharuki na uhasama. Wanajeshi vamizi wa Marekani wanachukua hatua za uhasama, ikiwa ni pamoja na kuunda maeneo yenye mamlaka ya ndani nchini Syria na kuyahimiza kujitenga.

Moscow inaamini kuwa Washington sio tu inaendelea kukwamisha utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Syria, bali pia inayatumia makundi ya kigaidi kama chombo na kuyachochea kupambana na serikali halali ya Syria. Kuwepo majeshi ya Marekani nchini Syria ni hatua isiyo halali na kinyume na  sheria za kimataifa, haswa ukiukaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na ukiukwaji wa wazi wa uhuru wa kitaifa na mamlaka ya kujitawala Syria.

342/