Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

3 Aprili 2023

14:57:36
1355850

Kukiri Biden kuhusu kutenga serikali ya Marekani bajeti kwa ajili ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi zingine

Rais Joe Biden wa Marekani amesema kuwa, nchi hiyo imetenga bajeti ya mabilioni ya dola ambayo yatatumika katika masuala ambayo ameyataja kama “kuufanya mwenge wa uhuru uendelee kuwaka”.

Biden amesema hayo katika hotuba yake aliyoitoa katika “Mkutano wa Demokrasia” ambao umefanyika kwa njia ya mawasiliano ya intaneti.

Rais Biden ametangaza kuwa, Marekani itatumia kiasi kingine cha dola milioni 690 katika masuala ambayo amesema ni juhudi za Washington kwa ajili ya kuunga mkono demokrasia katika maeneo tofauti ya dunia. Biden amesema ana mpango wa kuomba kiasi kingine cha dola bilioni 9.5 kutoka kwa Kongresi ya nchi hiyo kwa ajili ya kufanikisha mpango huo.  Kwa mujibu wa Biden, kiasi kikubwa cha fedha hizo kitapatiwa idara mpya ambayo itaanzishwa ndani ya Taasisi ya Ustawi wa Kimataifa. Taasisi hii inafanya kazi zake chini ya usimamizi wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani na kidhahiri lengo lake ni kutekeleza mipango ya kibinadamu. Biden amesema, dunia yetu inahitajia demokrasia yenye nguvu zaidi na mwenge wa uhuru uendelee kuwaka kwa ajili ya yetu na kizazi kijacho.

Hatua ya Joe Biden ya kukiri kuhusu kutengwa bajeti kubwa kwa ajili ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi zingine kwa mara nyingine tena hilo limeweka wazi sura halisi ya Marekani. Tangu kuanzia kipindi cha vita baridi hadi sasa, Marekani daima imekuwa ikiingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine katika fremu ya malengo na maslahi yake pamoja na washirika wake kama Uingereza. Marekani ikiwa na nia ya kufikia malengo yake hayo, siyo tu kwamba, imeanzisha vita na kupanga na kutekeleza mapinduzi katika maeneo tofauti ya dunia, bali imeunga mkono moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja vyama, harakati, wanasiasa, asasi zisizo za kiserikali na vyombo vya habari vyenye mfungamano na Wamagharibi. 

Katika uwanja huu, sambamba na kufanyika mkutano wa demokrasia, ikulu ya White House imetoa ripoti ambayo inaonyesha kutengwa bajeti mpya na serikali ya Washington kwa ajili ya kile kinachoelezwa kuwa eti ni kueneza demokrasia. Ndani ya ripoti hiyo kumetajwa mataifa ambayo bajeti hiyo itatumika kwa ajili ya kueneza demokrasia hiyo. Serikali ya Marekani imedai kwamba, fedha za walipa kodi wa nchi hiyo ndizo zitakazosaidia kuimarisha demokrasia katika mataifa mengine na kwamba, fedha hizo zitatumika katika masuala kama kuunga mkono vyombo huru vya habari, kuimarisha suala la kutangaza habari sahihi, kukabiliana na ufisadi, kuimarisha haki za binadamu, kufanyia mageuzi demokrasia na kutetea uchaguzi huru, salama na wa amani.

Katika hali ambayo, Marekani inajitangaza kuwa kinara wa kutetea demokrasia ulimwenguni, haifahamiki ni asasi gani ya kimataifa ambayo imeiteua Washington na kuiona kuwa inastahiki kubeba jukumu hilo. Ni nani aliyeipatia serikali ya Biden jukumu hili la kueneza demokrasia na kutoa maoni na mtazamo kuhusiana na hali ya demokrasia katika mataifa mengine ya dunia?

Fauka ya hayo, kama ilivyokuwa katika madai ya haki za binadamu ya Marekani, madai ya Washington kwamba, nchi hiyo ndio iliyopiga hatua zaidi ulimwenguni katika uga wa demokrasia na kwamba, inashikilia uongozi wa hilo ni kichekesho na kioja. 

Hata wajuzi na wasomi wa Kimarekani wenyewe hawakubaliani na mtazamo huo. Profesa Stephan Walt, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani na mwananadharia mahiri wa nchi hiyo anasema: Filihali Marekani haina sifa wala ustahiki wa kuongoza kikao kama hiki cha “mkutano wa demokrasia. Kabla ya uchaguzi wa Rais 2020 kituo cha taarifa za kiuchumi kiliiweka Marekani katika orodha ya nchi zenye demokrasia yenye mapungufu. Kadhalika moja ya vyama vikuu vya nchi hiyo kilikataa kutambua matokeo ya uchaguzi na baadhi ya wafuasi wa chama cha Repulican wanafunika shambulio dhidi ya Kongresi ya nchi hiyo. Kama tunafanya hima kwa ajili ya kuwa kiongozi wa demokrasia, masuala kama haya yanakinzana na hilo."

Matamshi hayo ya mwananadharia huyo wa Kimarekani yanaashiria tukio la kushambuliwa Kongresi ya Marekani lililofanywa na wafuasi wa Donald Trump Rais wa zamani wa nchi hiyo wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Novemba 2020. 

Trump amewahi kunukuliwa mara kadhaa akisema kwamba, demokrasia nchini Marekani ni uongo mtupu. Hatua yake ya kuutaja mfumo wa uchaguzi nchini Marekani kwamba, ni ufisadi na kutoa tuhuma za kutokea wizi na uchakachuaji katika uchaguzi wa nchi hiyo ni jambo ambalo lilipelekea kuibuka mgogoro wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa katika nchi hiyo na hivyo kutilia shaka demokrasia ya nchi hiyo inayopigiwa upatu.

Kwa msingi huo, pamoja na madai ya Marekani kuhusiana na kuwa kiongozi wa demokrasia ulimwenguni, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, kwa muda mrefu sasa demokrasia imekuwa haina maana yake halisi katika uga wa kijamii na kisiasa nchini Marekani.