Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

7 Aprili 2023

14:51:32
1356636

Mkuu wa CIA: Marekani imesikitishwa na kuboreka uhusiano wa Saudia na Iran, Syria

Mkurugenzi wa Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani, CIA, William Burns ameripotiwa kusikitishwa na hatua ya Saudi Arabia kufikia mapatano ya kurejesha uhusiano na Iran na Syria huku weledi wa mambi wakiashiria kupungua kwa ushawishi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal, mkuu huyo wa ujasusi nchini Marekani alisafiri hadi Riyadh katika muda usiojulikana wiki hii ili kuzungumzia ushirikiano wa kijasusi.

Wakati wa mkutano na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Mohammed Bin Salman, Burns alilalamika kwamba Washington inahisi "imepuuzwa" katika mchakato wa Saudia wa kurejesha uhusiano na Iran na Syria.

Alielezea kufadhaika kwa Marekani kwa kuachwa nje ya matukio ya kikanda. Kuvurukigka uhusiano wa nchi za eneo kumekuwa kwa maslahi ya Marekani kwani kwa njia hiyo imeweza kuendelea kuwa na ushawishi katika nchi za Kiislamu lengo lake kuu likiwa ni kuzidhoofisha.

Iran na Saudi Arabia zilikubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia Machi 10 baada ya mazungumzo magumu  chini ya upatanishi wa China mjini Beijing.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili walifanya mkutano wa kihistoria siku ya Alhamisi mjini Beijing kuashiria kurejeshwa rasmi kwa uhusiano.

Katika taarifa ya pamoja pande hizo zilisisitiza haja ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na kuainisha mpango wa kuimarishwa kwa ushirikiano na kuimarisha usalama wa kikanda. Pia waliahidi kuchukua hatua zinazohitajika ili kufungua tena balozi na ofisi za kidiplomasia.

Wanadiplomasia wakuu wa Iran na Saudi pia wametoa shukrani kwa Beijing kwa kuandaa mkutano wao huku waangalizi wakiashiria kuongezeka kwa ushawishi wa China katika eneo huku kukiwa na kuzorota nafasi Marekani.

Tehran na Riyadh zimeonyesha kuwa na nia ya dhati juu ya kurejeshwa kwa uhusiano huku Rais wa Iran Sayyid Ebrahim Raisi akikubali mwaliko kutoka kwa Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdulaziz Al Saud kutembelea Riyadh.

Katika mabadiliko mengine ya sera za kigeni, Saudi pia imechukua hatua za kurejesha uhusiano na Syria huku Marekani ikionekena kupinga hatua hiyo. Saudia halikadhalika imemwalika Rais wa Syria Bashar al-Assad kwenye mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mwezi Mei.

Kwa mujibu wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Mwanamfalme Faisal bin Farhan anatarajiwa kusafiri hadi Syria katika wiki zijazo ili kuwasilisha binafsi mwaliko rasmi kwa Rais Assad.

342/