Main Title

source : Parstoday
Jumapili

23 Aprili 2023

17:35:55
1359903

Mgombea urais wa chama tawala cha Democratic akiri: Marekani ndiyo iliyounda kundi la kigaidi la Daesh

Robert F. Kennedy Jr ambaye ametangaza nia yake ya kugombea katika uchaguzi wa urais mwaka ujao nchini Marekani, amekiri kwamba nchi hiyo ndiyo iliyounda kundi la kigaidi la Daesh (ISIS).

Robert F. Kennedy Jr mwenye umri wa miaka 69, mpwa wa rais wa zamani wa Marekani, John F. Kennedy, amesema: "Polisi wa nchi hii ni wafisadi, tulitengeneza kundi la kigaidi la ISIS na tumetuma wakimbizi milioni 2 Ulaya na kuyumbisha demokrasia barani humo, hali iliyosababisha Brexit na kujiondoa Uingereza katika umoja wa Ulaya."

Mwanasiasa huyo wa chama cha Democratic na mshindani wa Joe Biden ameongeza kuwa, hii ni sehemu ya gharama za vita vya Iraq vilivyotumia jumla ya dola trilioni 24.

Kennedy amesisitiza kuwa, gharama hizo hazikuwa na faida yoyote isipokuwa uharibifu kwa tabaka la kati la Marekani na kuna ulazima wa kukomeshwa hali hii. Katika awamu ya kwanza ya kampeni zake za uchaguzi, Robert Kennedy ameweza kuvutia idadi kubwa ya wapiga kura wa Biden na kupata uungaji mkono wao.

Kukiri kwa mwanasiasa huyo wa ngazi za juu wa Marekani, ambaye anataka kuingia Ikulu ya White House na kushika wadhifa wa Rais, kwamba nchi hiyo ilihusika moja kwa moja katika uundaji wa kundi la kigaidi la Daesh, kwa mara nyingine tena kumefichua uongo wa Washington kuhusu madai yake ya kupambana na ugaidi, hususan kundi la kigaidi la ISIS. Vilevile kunaweka wazi nafasi ya Marekani katika uundaji na upanuzi wa kundi la ISIS ambalo limefanya jinai kubwa na za kutisha katika nchi za Syria, Iraq, Afghanistan na sehemu nyingine za dunia.

Hii si mara ya kwanza kwa mwanasiasa mtajika wa Marekani kufichua nafasi ya Washington katika kuunda kundi la kigaidi la ISIS. Rais wa zamani Marekani, Donald Trump pia aliwahi kufichua kwamba mtangulizi wake, Barack Obama, na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton ndio walioanzisha kundi la kigaidi la Daesh. Trump alisema katika hotuba yake ya kampeni za uchaguzi Januari 2016, kwamba: “Obama na Clinton sio waaminifu. Waliunda kundi la ISIS. Hillary Clinton pamoja na Obama ndio walioanzisha ISIS.”

Matamshi haya ya Trump kwa hakika yalikuwa uthibitisho wa shutuma ambazo zilikuwa zimetolewa mara nyingi na wakuu wa baadhi ya nchi za dunia, kama vile Rais wa Urusi Vladimir Putin, juu ya kuhusika moja kwa moja Ikulu ya White House katika uundaji wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS). Marekani ikishirikiana na waitifaki wake wa Kiarabu katika eneo la Magharibi mwa Asia, ilikuwa na nafasi kubwa katika kulianzisha na kuliendeleza kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ili kukabiliana na mhimili wa muqawama na mapambano, na imefanya juhudi za kuendelea kupanua shughuli za ISIS huko Iraq na Syria na kisha Afghanistan. Kuna ushahidi mwingi na wenye mashiko na hoja madhubuti katika uwanja huu. Kwa msingi huo, Marekani haiwezi kuficha au kufunika nafasi na mchango wake katika kuunda na kudumisha kundi hilo la kigaidi.

Awali wapiganaji wa kundi hilo la Daesh walikusanywa kutokana na mabaki ya makada wa chama cha Baath nchini Iraq, mawahabi na matakfiri kutoka maeneo mbalimbali ya dunia; na kisha kundi hilo likapanuliwa kwa kasi kubwa katika maeneo mbalimbali ya Syria. Marekani ilisaidiana na washirika wake wa Kimagharibi na Kiarabu katika kuunda kundi hilo. Lengo la kuanzishwa magenge kama haya ya kigaidi ni kuyatumia kama fimbo na silaha kwa ajili ya kutimiza mipango ya serikali ya Washington na mabeberu wenzake.

Suala jingine muhimu ni kwamba, Marekani na washirika wake ambao wana historia ndefu ya kuyasaidia na kuyafadhili makundi ya kigaidi kama ISIS, wanajinadi kuwa wako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Daesh kwa kuunda kile kilichoitwa muungano wa kupambana na ISIS Agosti 2014. Uongo huu umebainika na kuonekana waziwazi kwa walimwengu.

Kuanzia mwaka 2011 hadi katikati ya 2014, Wamarekani walitoa msaada mkubwa kwa kundi la ISIS na walikuwa na mchango mkubwa katika kutoa misaada ya kilojistiki na ufadhili kwa kundi hilo. Hapana shaka yoyote kwamba, bila ya msaada huo wa Washington, ISIS kamwe isingeweza kufanya uhalifu mkubwa kama ule ulioshuhudiwa Iraq na Syria.Hata katika kipindi cha sasa pia, Washington inaamini kwamba, itaweza kutumia mabaki ya magaidi wa ISIS kama nyenzo na silaha dhidi ya serikali za Syria na Iraqi na washirika wao wakati wowote, ili kuwawekea mashinikizo. Kwa msingi huo imekuwa ikiwapa silaha, mafunzo na misaada ya kifedha magaidi hao na hata kuwafungua kutoka jela wafungwa wa ISIS na kuwaruhusu kutekeleza operesheni za kigaidi kwa niaba yake.

342/