Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

4 Mei 2023

12:02:01
1362642

Morocoo yatambua kuanza Mwaka Mpya wa Maberiberi kuwa siku rasmi ya mapumziko

Siku ya kuanza Mwaka Mpya wa jamii ya Amazigh au Maberiberi imetangazwa kuwa siku rasmi ya mapumziko nchini Morocco, katika hatua mpya iliyochukuliwa na Mfalme Mohammed VI kuitambua jamii hiyo ya Wenyeji wa nchi hiyo ambayo imefanya kampeni kwa miaka mingi kutaka kalenda yao itambuliwe rasmi.

Taarifa rasmi iliyotolewa na ofisi ya mfalme Mohammed VI imesema, kiongozi huyo ameamua kuitangaza Siku ya Mwaka Mpya wa Maberiberi siku ya taifa ya mapumziko rasmi yenye malipo.

Mwaka Mpya wa jamii ya Amazigh huadhimishwa Januari 13. Siku ya kwanza ya mwaka katika kalenda ya Amazigh, inayotokana na misimu na kilimo, inaadhimisha kumbukumbu ya kutwaa Mfalme Sheshonq wa Libya kiti cha enzi cha Misri, kulingana na wanahistoria.

Siku hiyo pia huadhimishwa na Wamorocco wanaozungumza Kiarabu ambao huiita mwanzo wa mwaka wa kilimo.

Waberiberi wanaishi katika eneo linaloenea sehemu kubwa ya Afrika Kaskazini, lenye idadi kubwa ya watu nchini Morocco, Algeria, Tunisia, Libya na magharibi mwa Misri. Lakini mbali na huko, makabila ya Waberiberi na makundi ya makabila hayo yanapatikana pia kusini mwa Niger, Mali na Burkina Faso. Neno Tamazight linamaanisha wigo wa lahaja mbalimbali zinazozungumzwa na Waberiberi.

Morocco, ambayo ni makazi ya idadi kubwa zaidi ya Waamazigh au Waberiberi kaskazini mwa Afrika iliitenga lugha na utamaduni wa jamii ya Waberiberi kwa muda mrefu na kuzipa upendeleo zaidi lugha za Kiarabu na Kifaransa, na hivyo kusababisha vuguvugu la kupigania utambulisho wa Amazigh ambalo limepata kasi kubwa ya ushawishi.

Madai ya vuguvugu la Amazigh yalipamba moto zaidi katika maandamano ya mwaka 2011, ambayo yalipelekea Morocco kupitisha katiba mpya na mfalme wa nchi hiyo kukabidhi baadhi ya mamlaka yake kwa serikali iliyochaguliwa na wananchi.../

342/