Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

6 Mei 2023

16:45:10
1363203

Ujerumani: Tunaunga mkono Afrika iwe mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la UN

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amesema nchi yake inaunga mkono mpango wa bara la Afrika kuwa na uwakilishi wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Akiwa katika ziara ya siku mbili nchini Kenya, Scholz amemueleza Rais wa nchi hiyo William Ruto kwamba anaamini matatizo ya Afrika yatasuluhishwa kwa uongozi wa nchi za Afrika, akitoa mfano wa mapigano yanayoendelea nchini Sudan.

Aidha amesema, Ujerumani inaunga mkono wazo la Afrika kuwa mwanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na kupewa nafasi Umoja wa Afrika kuwa na mwakilishi kwenye kundi la nchi tajiri 20 duniani G-20.

Wakati mabara ya Amerika, Ulaya na Asia yana nchi ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bara la Afrika ndilo pekee ambalo halina uwakilishi wa uanachama wa kudumu kwenye chombo hicho chenye sauti ya juu ndani ya umoja huo.

Pendekezo la Umoja wa Afrika kuwa na nafasi katika mikutano ya nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi, G20 lilitolewa kwa mara ya kwanza na  Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.

Kabla ya ziara yake nchini Kenya iliyomalizika leo, siku ya Alkhamisi, Kansela wa Ujerumani alitembelea Ethiopia na kufika makao makuu ya Umoja wa Afrika AU, ambako alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Kamisheni ya umoja huo Moussa Faki Mahamat. 

Katika mazungumzo yake na mkuu wa kamisheni ya AU, Scholz alisema Afrika inapaswa kuwa na masuulia makubwa zaidi katika masuala ya kimataifa na akaahidi kwamba Ujerumani itaunga mkono matakwa ya Umoja wa Afrika kuweko katika mikutano ya kundi la G20.../

342/