Main Title

source : Parstoday
Jumapili

7 Mei 2023

12:05:48
1363497

Serikali ya Samia yafufua mchakato wa Katiba, atoa maagizo kwa Baraza la Vyama vya Siasa

Siku chache baada ya Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Dk Damas Ndumbaro kutangaza kuanza mchakato wa Katiba Mpya uliokwama, Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuitisha kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa.

Baraza hilo limetakiwa kukutana ili kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu mbalimbali kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Rais Samia alitoa agizo hilo jana Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma alipofanya kikao na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Jaji Mutungi na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama na Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro.

Mbali ya mchakato wa Katiba, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi, zikiwemo sheria za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Msajili wa vyama vya Siasa.

Lengo la kuitishwa kwa Baraza hilo linaloshirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu ni kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu mbalimbali kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Kikosi kazi hicho kilichokuwa kikiongozwa na Mwenyekiti, Profesa Rwekaza Mukandala pamoja na mambo mengine, kilipendekeza mchakato wa Katiba uliokwama mwaka 2014 kwa hatua ya Katiba Pendekezwa kufufuliwa.

342/