Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

8 Mei 2023

10:27:57
1363781

Waliofariki dunia kwa janga la mafuriko DRC sasa ni zaidi ya 400

Idadi ya watu walioaga dunia kufuatia janga la mafuriko na maporomoko ya udongo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeongezeka kupindukia 400.

Takwimu hizo mpya za maafa ya mafuriko DRC zinaonyesha pia kuwa, watu wengi zaidi bado hawajulikani walipo na hivyo kuna uwezekano wa kuongezeka idadi ya vifo.

Takriban miili 400 imeopolewa kufuatia mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyokumba vijiji viwili mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika vijiji kadhaa vilivyo karibu na ufuo wa Ziwa Kivu, watu wamekuwa wakichimba tope kwa mikono katika harakati za kuwatafuta jamaa waliopotea.

Wafanyakazi wa kujitolea wa Msalaba Mwekundu wa Congo hawana mifuko ya kuhifadhi miili. Wanalazimika kuirundika miili iliyofunikwa kwa blanketi katika vijiji vya Bushushu na Nyamukubi katika jimbo la Kivu Kusini.

Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba katika mojawapo ya vijiji vya Kivu Kusini zaidi ya robo tatu ya nyumba zote zimesombwa na maji ikiwa ni pamoja na vituo vya afya na shule.

Upande wa pili wa Ziwa Kivu katika nchi jirani ya Rwanda wasiopungua 136 wameripotiwa kuaga dunia kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo.

Nyumba zisizopungua 500 pia zimeharibiwa na mafuriko ya wiki hii nchini Rwanda hususan katika Wilaya za Rubavu, Karongi, Rutsiro, Nyabihu na Ngororero ambazo ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo.

Janga hilo la mafuriko limeikumba pia nchi jirani ya Uganda ambapo taarifa kutoka nchini humo zinasema, mbali na baadhi ya barabara kuharibiwa katika baadhi ya maeneo, kwa akali watu 20 wameriipotiwa kuaga dunia kwa mafuriko hayo.

342/