Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

12 Juni 2023

20:01:12
1372615

Ripoti: Mamilioni ya watoto wanatumikishwa duniani, hasa Afrika

Shirika la Kazi Duniani (ILO) limesema mamilioni ya watoto hasa katika nchi maskini dunia wanatumikishwa, huku likitahadharisha kuhusu kuongezeka utumwa mamboleo duniani.

Shirika hilo la kufuatilia masuala ya ajira la Umoja wa Mataifa limesema hayo katika taarifa iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kutumikishwa Watoto inayoadhimishwa leo Juni 12 kote duniani. 

Ripoti ya Shirika la ILO pamoja na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) imeeleza kuwa, mtoto mmoja kati ya watano analazimika kutumika katika kazi za kulazimishwa, na zaidi ya nusu ya watoto hao wametumbukia katika biashara ya utumwa wa ngono barani Afrika. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jumla ya watoto milioni 160 wanatumishwa katika maeneo mbalimbali duniani, hususan katika nchi za eneo la chini ya jangwa la Sahara barani Afrika. Ripoti hiyo imesema watoto milioni 97 wa kiume na milioni  63 wa kike wanatumikishwa kote dunia.

Mapema mwezi huu, Shirika la Save the Children lilisema mamia ya mamilioni ya watoto wanaishi katika maeneo yenye migogoro ya kivita na wanakabiliwa na hatari ya kifo.

Ripoti hiyo ya Juni 4 ilisema kufikia mwaka 2021, watoto wasiopungua milioni 449 walikuwa wanaishi katika maeneo ambayo yana makundi ya wabeba silaha na vikosi vya serikali ambavyo vinasajili watoto kuingia vitani. Imesema katika kipindi hicho, kesi 24,000 za unyanyasaji wa kuchupa mipaka dhidi ya watoto zilinakiliwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), sababu kubwa ni umaskini kwenye familia ambao husababisha wazazi kutumia watoto wao kufanya kazi kwenye sekta ya kilimo.

FAO imesema watoto wanapotumikishwa hasa kwenye kilimo mbali na kushindwa kwenda shule, watoto wanakuwa wanakumbwa na madhara ya kiafya kutokana na kemikali zinazotumika kwenye sekta ya kilimo na mara nyingi wazazi hutumia watoto wao kwa kuwa wanafanya kazi bila ujira.

342/