Main Title

source : Parstoday
Jumatano

14 Juni 2023

13:28:59
1373025

UNHCR: Watu milioni 110 walazimika kukimbia makazi yao

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema takribani watu milioni 110 wameyakimbia makazi yao kutokana na mizozo, mateso, njaa, ukiukaji wa haki za binaadamu na mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti iliyotolewa leo Jumatano na Kamishna Mkuu wa Shirika la UNHCR, Filippo Grandi, imeeleza kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2022, idadi ya watu wasio na makaazi ilikuwa milioni 108.4.

Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva, Grandi amesema katika ujumla wa kimataifa, watu milioni 35.3 ni wakimbizi, watu waliovuka mipaka ya kimataifa kutafuta usalama, huku watu milioni 62.5 wakilazimika kuwa wakimbizi wa ndani ya nchi zao kutokana na mizozo na ghasia.

Grandi amesema, vita nchini Sudan imesababisha watu wapatao milioni 2 kuyakimbia makaazi yao tangu mwezi Aprili, na kuifanya hiyo kuwa idadi iliyovunja rekodi.

"Watu wengi wanaokimbia, hawakimbilii kwenye nchi tajiri, lakini kwenye nchi ambazo ni za kipato cha chini au cha kati, ambao ni takribani asilimia 76," alifafanua Grandi.

Ripoti hiyo kuhusu mwelekeo wa dunia ya UNHCR imeeleza kuwa, mwaka jana pekee, zaidi ya watu milioni 19 walilazimika kuyakimbia makaazi yao, ikiwa ni pamoja na zaidi ya milioni 11 waliokimbia vita nchini Ukraine katika kile kilichotajwa kuwa uhamiaji wa haraka na mkubwa zaidi wa watu kuwahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

UNHCR imesema hali ya ongezeko hilo haioneshi dalili za kupungua kwa mwaka 2023, kwani hadi mwezi Mei, mgogogoro nchini Sudan ulisababisha idadi jumla kimataifa kufikia wastani wa milioni 110.

Mwaka 2022, mizozo kwenye nchi za Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Myanmar pia ilichangia kuwalazimisha zaidi ya watu milioni moja kuyakimbia makaazi yao katika kila nchi.

342/