Main Title

source : Parstoday
Jumatano

14 Juni 2023

13:29:51
1373026

Trump amshambulia Biden, asema ni fisadi na akishinda atampandisha kizimbani

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, amemshambulia Rais wa sasa wa nchi hiyo, Joe Biden, akimtuhumu kuwa ni fisadi, na ameahidi kumfungulia mashtaka mahakama. Trump ameyasema hayo saa chache baada ya kumalizika kikao cha kwanza cha kesi yake katika kile kinachojulikana kama kesi ya hati za siri.

Katika hotuba aliyoitoa jana jioni, Jumanne kwa saa za Marekani, mbele ya umati wa wafuasi wake huko New Jersey, Trump alisema kuwa Biden ataarifishwa kama rais fisadi zaidi wa Marekani.

Ameongeza kuwa inasikitisha kuona "rais fisadi" akijaribu kumkamata mpinzani wake wa kisiasa kwa kile alichokiita "tuhuma za uwongo".

Donald Trump amedai kwamba iwapo atachaguliwa kuwa rais, atamteua “mwendesha mashitaka halisi wa umma” kumfuatilia Biden, na atafuta kile alichokitaja kuwa ni hali ya kina inayotaka kumnyima uhuru wake. Amesema: “Hatuna tena demokrasia nchini Marekani ambako mpinzani wa kisiasa anakamatwa, na nchi yetu iko katika hali ya hatari."

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, rais huyo wa zamani wa Marekani amesema kuwa iwapo atashinda uchaguzi ujao nchini humo atamaliza vita kati ya Russia na Ukraine ndani ya saa 24, ahadi ambayo aliikariri katika miezi kadhaa iliyopita.

Itakumbukwa kuwa, jana, rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alifikishwa mbele ya mahakama ya Miami, Florida, kujibu tuhuma zinazomkabili kuhusiana na kuhifadhi, kinyume cha sheria, nyaraka zinazohusiana na usalama wa taifa alipoondoka madarakani, pamoja na kuwadanganya maafisa waliotaka kuzirejesha nyaraka hizo.

Ndani ya taratibu za kisheria zinazotumika, rais huyo wa zamani alikamatwa akiwa na msaidizi wake kwa dakika 10, na chanzo cha mahakama kilisema kuwa Trump atahukumiwa kama watuhumiwa wengine. Alisema kuwa taratibu hizo ni pamoja na kuchukua alama za vidole vyake kidijitali na kuweka picha yake kwenye kumbukumbu za mahakama, lakini haitachapishwa kwa umma.

Donald Trump ndiye rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kukabiliwa na kesi ya jinai ya Shirikisho baada ya muda wake kumalizika, lakini hiyo sio kesi pekee inayomsubiri.

342/