Main Title

source : Parstoday
Jumatano

14 Juni 2023

13:39:33
1373040

Sekretarieti ya EAC yawasilisha makadirio ya bajeti yake

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imewasilisha makadirio ya bajeti kwa bunge la jumuiya hiyo.

Taarifa zaidi kutoka ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaeleza kuwa, makadiriol ya bajeti hiyo ni dola za Kimarekani zaidi ya milioni miamoja na tatu, kwa mwaka wa fedha 2023-2024.

Katika hotuba yake ya uwasilishwaji wa bajeti hiyo, mwenyekiti wa mawaziri wa jumuiya hiyo Ezechiel Nibigira raia wa Burundi, amebainisha kwamba, makadirio ya bajeti ya mwaka huu yanawasilishwa wakati uchumi wa jumuiya hiyo kongwe barani Afrika, ukiwa mashakani kutokana na misukosuko mbalimbali ya kimataifa kama vita na mabadiliko ya tabianchi.

Hotuba hiyo iliyosomwa katika makao makuu ya jumuiya ya Afrika Mashariki mkoani Arusha kaskazini mwa Tanzania pia ilibainisha kwamba, pamoja na changamoto hizo, lakini ukuaji wa uchumi katika ukanda huo uliimarika kwa asilimia 4. 8 mwaka 2022, kutoka asilimia 3.5 mwaka juzi (2021).

Taarifa zaidi zinasema kuwa, bajeti hiyo imezingatia maeneo tisa ya vipaumbele, ikiwapo uimarishaji wa michakato ya utawala wa kikanda, uboreshaji wa mifumo ya forodha pamoja na usimamizi wa mifumo ya amani ya kikanda na kimataifa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni nnchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilikubaliana kuondoa gharama ya viza baina yao.

Makubaliano hayo yalimefikiwa katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCTIFI) uliofanyika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Jijini Arusha Tanzania ambapo viliainishwa vikwazo vichache vilivyoondolewa huku vingine vikiendelea kufanyiwa marekebisho.

342/