Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

16 Juni 2023

10:50:37
1373469

UN: Zaidi ya 100 wameuawa katika mapigano Darfur Kaskazini, Sudan

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema watu zaidi ya 100 wameuawa kwenye mapigano katika jimbo la Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan.

Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa UNHCR alisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, mapigano mabaya katika kambi za wakimbizi wa ndani katika jimbo hilo, yamepelekea kuuawa watu wasiopungua 100, mbali na wengine wengi kujeruhiwa.

Ameeleza kuwa, UNHCR kadhalika imepokea ripoti za kufanyika unyanyasaji mkubwa wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana ndani na pambizoni mwa kambi za IDPs kwenye jimbo hilo lililoko magharibi mwa Sudan. 

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, iwapo pande hasimu hazisitisha mapigano hayo, hali ya kibinadamu katika eneo hilo itakuwa mbaya zaidi.

Hii ni katika hali ambayo, juzi Jumatano jeshi la Sudan liliwatuhumu wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kuwa walimteka nyara na kumuuwa Gavana wa jimbo la Darfur Magharibi, Khamis Abdallah Abakar; na kuyataja mauaji hayo kuwa ni "kitendo cha kinyama."

Umoja wa Mataifa pia umetoa taarifa ya kulaani mauaji hayo. Vita kati ya majenerali hasimu huko Sudan jana Alhamisi viliingia katika mwezi wake wa tatu na haijulikani lini vitamalizika. 

Vita hivyo vilivyoanza Aprili 15 baina ya wanajeshi wa serikali chini ya Kamanda wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah al Burhan na hasimu wake Kamanda Mohamed Hamdan Dagalo anayeongeza RSF hadi sasa vimeuwa karibu watu 1,000.

342/