Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

16 Juni 2023

10:51:18
1373470

Mahakama ya ICC kuchunguza jinai za kivita mashariki ya DRC

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imesema itachunguza madai ya kufanyika uhalifu wa kivita huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Karim Khan, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC na kuongeza kuwa, "Napanga kufanya uchunguzi wa awali kwa kina, kufuatia ombi la serikali ya Kinshasa."

Serikali ya Kinshasa inalituhumu kundi la waasi la M23 kuwa linafanya mashambulizi ya mara ya mara katika mkoa wenye utajiri mkubwa wa madini wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi.

Aidha DRC imekuwa ikiituhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi hilo la wabeba silaha, madai ambayo yamekanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Mapema mwezi huu,  DRC na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ziliafikiana kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na hatua ya kutochukuliwa sheria watu wanaohusishwa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Mahakama ya ICC yenye makao yake mjini Hague nchini Uholanzi imekuwa ikifuatilia Kongo tangu mwaka 2002 na ilianzisha uchunguzi wake wa kwanza kaskazini Mashariki mwa jimbo la Ituri mwaka 2004.

Tayari Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mbabe wa zamani wa vita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Bosco Ntaganda baada ya kumpata na hatia ya kufanya ukatili ikiwa ni pamoja na kuua, kubaka na kuwatumikisha watoto kama askari vitani.

342/