Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

16 Juni 2023

10:52:06
1373471

Ombi la Misri la kujiunga na BRICS; ishara ya kupunguza uhusiano wake na nchi za Magharibi

Ikiwa ni katika mwenendo wa nchi za dunia kuvutiwa na miungano pamoja na mashirika yasiyofungamana na Marekani na nchi nyingine za Magharibi, Misri imeomba uanachama katika jumuiya ya BRICS.

Misri inataka kuimarisha uhusiano wa kibiashara na ushirikiano wa kiuchumi na Russia katika hali ambayo Marekani inatoa mashinikizo makubwa kwa lengo la kuzizuia nchi mbalimbali duniani kushirikiana na Moscow. Kuhusiana na suala hilo, balozi wa Russia nchini Misri, Georgy  Borisenko amesema kwamba Misri imewasilisha ombi lake la kutaka kujiunga na kundi la BRICS kwa sababu moja ya jitihada zinazofanywa na kundi hilo ni kuwezesha biashara kufanyika kwa kutumika sarafu isiyokuwa dola ya Marekani, yaani sarafu za nchi wanachama au sarafu ya pamoja kati ya nchi hizo.

 Amesema juhudi za Misri kuimarisha uhusiano wake na Moscow zinafanyika katika hali ambayo Marekani imeongeza juhudi za kimataifa za kutaka kuitenga Russia. Ameashiria kuwa hivi karibuni Cairo ilikataa ombi la Washington la kufunga anga yake kwa ndege za Russia.

Kutokana na uhusiano mzuri na unaozidi kupanuka kati ya Misri na Russia, Marekani imejaribu kila mara, hasa katika miaka ya hivi karibuni, kutumia sera ya fimbo na karoti, yaani sera ya vitisho na ushawishi, na hasa kwa kutumia kadi ya "msaada wa kijeshi wa  kila mwaka wa Marekani kwa Misri" ili kuishawishi Cairo kukata uhusiano wake na Moscow.

Hata hivyo, juhudi hizo zimepingwa na Misri. Uamuzi wa Cairo wa kudumisha uhusiano wake na Russia na wakati huo huo kujaribu kujiunga na taasisi na mashirika yasiyo ya Kimagharibi umepelekea baadhi ya wachambuzi kutathmini uamuzi huo kuwa ni hujudi za kujitenga na nchi za Magharibi.

Ombi la Misri la kujiunga na BRICS lilitangazwa katika hali ambayo mawaziri wa mambo ya nje wa BRICS walikuwa wanafanya mkutano wao mjini Cape Town tarehe 2 Juni. Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini ndizo wanachama wakuu wa kundi la BRICS, na jina la kundi hilo linatokana na herufi za kwanza za majina ya nchi hizo tano.

Wanadiplomasia wakuu wa nchi 12 zinazotaka kujiunga na BRICS pia walihudhuria mkutano huo. Argentina, Bangladesh, Comoro, Cuba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Gabon, Indonesia, Iran, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu na Venezuela zinataka kujiunga na BRICS.

Mnamo mwaka 2009, madola yanayoinukia kiuchumi duniani yalijaribu kuanzisha umoja wa kisiasa na kiuchumi kwa ajili ya ushirikiano bila ya uwepo wa madola ya Magharibi, na huo ndio ukawa mwanzo wa kubuniwa kundi la BRICS.

Kwa kuwa katika kilele cha kundi la BRICS, China na Russia zinafanya jitihada za kukomesha udhibiti wa sarafu ya dola na nguvu ya kiuchumi ya nchi za Magharibi katika mahusiano ya kibiashara kimataifa. Baada ya kupita muda, sasa nchi nyingine zinazostawi pia zimeonyesha hamu ya kujiunga na kundi hilo la kiuchumi.

Kundi la BRICS ni kielelezo cha nia ya nchi tano wanachama wa kundi hilo ambapo wanachama wake wanne yaani China, India, Brazil na Afrika Kusini, ni nchi zinazoinukia kiuchumi, kushiriki katika usimamizi wa uchumi wa dunia na kushindana na kundi la G7, ambalo linajumuisha nchi zilizoendelea kiviwanda za kambi ya Magharibi.

Kuhusiana na suala hilo, Russia inawataka wanachama wa kundi la BRICS kuchukua hatua za kurekebisha mfumo wa fedha na uchumi duniani, ili nchi zinazoendelea zipate fursa ya kuimarisha uchumi wao katika mazingira mazuri na ya kiadilifu.

Kundi la BRICS linajumuisha zaidi ya asilimia 40 ya watu wote duniani na lilianza kufanya kazi miaka 14 iliyopita kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kati ya nchi zinazoendelea na pia kuunda taasisi za kimataifa kama benki za maendeleo na mfumo mpya wa biashara kwa lengo la kuweza kushindana kiadilifu na taasisi nyingine kama hizo ulimwenguni.

BRICS ina rasilimali na uwezo mkubwa wa kuiwezesha kufikia maendeleo ya haraka ya kiuchumi na hivyo kuwa nguzo muhimu na yenye ushawishi na maamuzi makubwa katika uchumi wa kimataifa. Suala hili limeichochea Russia daima kutafuta njia za kuimarisha na kupanua wigo wa shughuli za kundi hili, na bila shaka Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo ana nafasi muhimu katika uwanja huo.

Putin anasisitiza kuwa nchi wanachama wa BRICS zinapaswa kusaidiana ili kuondoa kasoro zilizopo katika mfumo wa fedha duniani na kufutilia mbali matumizi ya sarafu maalum hasa dola ya Marekani katika mabadilishano ya kibiashara na akiba ya nje ya pesa zao. Amewaomba wanachama wa BRICS wachukue hatua madhubuti kwa ajili ya kurekebisha mfumo wa fedha na uchumi wa dunia ili kuziwezesha nchi zinazoendelea kustawi kiuchumi katika mazingira mazuri na ya haki.

Mehdi Khorsand, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, huku akisisitiza kwamba huenda pigo kubwa zaidi ambalo limetolewa na nchi za BRICS ni kwa mfumo wa kiliberali unaotawala dunia, amesema: BRICS, ambayo kwa mujibu wa wanauchumi itadhibiti nusu ya uchumi wa dunia katika muda wa chini ya miaka 10 ijayo, hatua yake ya kwanza imekuwa ni kupunguza nafasi na hisa ya dola katika mabadilishano ya kibiashara ya pande mbili na pande kadhaa kati ya nchi wanachama.

342/