Main Title

source : Parstoday
Jumanne

20 Juni 2023

08:48:30
1374182

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu: Tunalaani aina zote za ugaidi

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani shambulizi la kigaidi lililoua makumi ya wanafunzi katika eneo la Mpondwe, magharibi mwa Uganda na kusisitiza kuwa, taasisi hiyo inalaani kila aina ya ugaidi.

Shirika la habari la Anadolu limeinukuu Sekretarieti Kuu ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ikilaani mauaji hayo ya kigaidi nchini Uganda, na kuyataja kama jinai ya kihaini.

Taarifa ya jumuiya hiyo yenye makao yake mjini Jeddah imesisitiza kuwa, "Ni msimamo wetu wa daima kusimama dhidi ya aina na mifumo yote ya ugaidi."

OIC imesema katika taarifa yake hiyo kwamba, ipo tayari kuunga mkono na kushirikiana na mamlaka za Uganda kupambana na jinamizi la ugaidi.

Kadhalika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imetoa mkono wa pole familia za wahanga wa hujuma hiyo, serikali na taifa hilo kwa ujumla kufuatia shambulizi hilo la Ijumaa usiku lililoua makumi ya watu.

Vyombo vya usalama vya Uganda vimeimarisha ulinzi na tayari vimeanzisha msako mkubwa baada ya wanamgambo wenye silaha wa ADF wenye mfungamano na kundi la kigaidi ya Daesh (ISIS) kuwauwa watu wasiopungua 41, wengi wao wakiwa ni wanafunzi kwenye hujuma hiyo.

Mauaji hayo ya usiku wa kuamkia Jumamosi yalifanyika katika maeneo ya Magharibi mwa Uganda karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

342/