Main Title

source : Parstoday
Jumatano

21 Juni 2023

17:10:52
1374600

Umoja wa Mataifa wataka hatua za maana kuboresha hali ya wakimbizi

Umoja wa mataifa jana uliadhimisha siku ya wakimbizi duniani, wakati ambapo chuki dhidi ya wakimbizi zinaongezeka, na hivyo umoja huo unatoa wito kwa watu kuheshimu ujasiri na michango ya jamii za watu waliohamishwa kutoka makazi yao na vita, mateso, na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Siku ya wakimbizi duniani ya mwaka huu imeangazia hali mbaya ya wakimbizi milioni 35.4 na wanaotafuta hifadhi, juu ya mahitaji yao na haki za kisheria na usalama wao kote duniani.

Akizungumza kwenye hafla iliyofanyika katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, kambi kubwa duniani, Filippo Grandi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ameipongeza serikali ya Kenya kwa mipango yake ya “kutekeleza sera bunifu na inayojumuisha watu wote.”

Wakati huo huo, katika ujumbe wake maalumu wa kuadhimisha siku hii  ambayo ni Juni 20, Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amesema: Tunakabiliana na takwimu za kushangaza kwani “zaidi ya watu milioni 100 wanaoishi katika nchi zinazokumbwa na mizozo, mateso, njaa na machafuko ya mabadiliko ya tabianchi wamelazimika kuyahama makazi yao. 

Ameongeza kusema kuwa, siku hii “inatukumbusha wajibu wetu wa kulinda na kusaidia wakimbizi na wajibu wetu wa kufungua njia zaidi za msaada. Hii ni pamoja na suluhu za kuwapa wakimbizi makazi mapya na kuwasaidia kujenga upya maisha yao kwa utu.”

Kadhalika katika sehemu nyingine ya ujumbe wake kwa mnasaba wa Siku ya Wakimbizi Duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, wakimbiizi wanahitaji na wanastahili kuungwa mkono na mshikamano sio kukutana na mipaka iliyofungwa na kurudi nyuma walikotoka.

342/